Sifuna: Tuwe na umoja chamani ODM tukiomboleza Raila
CHAMA cha ODM kimeomba umoja kwa wanachama wake huku taifa likiendelea kumwombeleza kiongozi wao Raila Odinga.
Katibu Mkuu wa ODM, Edwin Sifuna, kwenye taarifa Jumatano alisema kuwa chama na uongozi wake bado kimeshtushwa na mauti ya Raila na la muhimu kwa sasa ni wao kuungana.
“Nawaomba wanachama waungane na waonyeshe umoja wakati huu ambapo tunatafakari kuhusu safari ya maisha na mauti ya kiongozi wetu, ambaye alikuwa mlezi wetu na baba wa wote,” akasema Bw Sifuna.
“Mheshimiwa Raila Odinga alikuwa msingi wa siasa zetu na mwingi wa kuwapa sisi matumaini,” akaongeza akimrejelea Bw Odinga kama mwanasiasa mzoefu ambaye alitawala mawanda ya kisiasa kwa zaidi ya miongo mitatu.
Alisema marehemu kiongozi huyo wa ODM alikuwa mpiganiaji wa demokrasia na aliwakuza hata viongozi wa sasa, mchango wake ukiacha alama ya kudumu katika siasa za Kenya.
“Atasalia nguli imara wa taifa letu na kipenzi cha Wakenya wengi kutokana na jinsi ambavyo alipigania nchi na kusimama imara kuhakikisha uhuru kwa kila mtu,” akasema Bw Sifuna.
Kwenye taarifa yake aliwataka wanachama wote waachane na tofauti zao za kisiasa na badala yake wawe na umoja kipindi hiki cha majonzi.
Aliongeza kuwa chama kinaendelea kushirikiana na familia na kitatoa mwelekeo kuhusu mipango ya mazishi.
“Tumakinikie maisha na mema ambayo kiongozi wetu alifanya wakati wa uhai wake huku tukiendelea kumwomboleza na kuhimili habari ya mauti yake,” akasema.
Kifo cha Raila kinatia kikomo taaluma ya kisiasa ambayo ilimshuhudia akidhibiti siasa za nchi huku akiwa kipenzi cha wengu kutokana na sera na msimamo wake wa kupigania mabadiliko ya uongozi wa nchi.