Habari za Kitaifa

Hii ndiyo ratiba ya Raila kutoka India hadi Bondo atakakozikwa Jumapili

Na CHARLES WASONGA October 15th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MWILI wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga utawasili nchini kutoka India saa mbili na nusu asubuhi Alhamisi, Oktoba 16, 2025 ambapo utapokelewa na Rais William Ruto katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenya (JKIA) huku akizikwa Jumapili, kwake Bondo, Siaya.

Katika uwanja huo wa ndege, Rais Ruto ataandamana na watu wa familia ya Raila, viongozi ODM na maafisa wakuu wa serikali, kulingana na taarifa iliyotolewa na Naibu Rais Kithure Kindiki Jumatano jioni.

Akihutubia taifa kutoka makazi yake rasmi mtaani Karen, Nairobi, Profesa Kindiki alifichua kuwa Odinga atazikwa kulingana na wosia wake “kwamba azikwe ndani ya saa 72 baada ya kifo chake.”

Hata hivyo, Profesa Kindiki aliyeandamana na nduguye Raila Dkt Oburu Oginga, alisema kuwa kwa sababu alifariki ng’ambo, mapenzi hayo yatabadilishwa kidogo kuingiliana na mahitaji ya mazishi ya kitaifa na desturi na tamaduni ya jamii yake.

“Baada ya mashauriano, imeagizwa kwamba Kamati Kuhusu Mazishi ya Kitaifa ioanishe wosia wa Raila pamoja na mahitaji ya kijamii na kiserikali,” akasema Profesa Kindiki ambaye pia aliandamana na mawaziri na viongozi wakuu wa ODM na maafisa wengine wa serikali.

“Tutafanya mambo haraka kwa saa na siku chache kwa sababu ya kile familia pamoja na wakili wa familia wametuambia. Tumearifiwa kwamba Raila alitaka azikwe saa 72 baada ya kifo chake,” Profesa Kindiki akaongeza.

Kulingana na Naibu Rais, japo Raila alikufa nje ya nchi, familia imekubali kuzingatia takwa lake “japo mabadiliko machache tu yatafanywa kuonisha taratibu za mazishi ya kitaifa na tamaduni za jamii yake.”

Baada ya mwili kuwasili, utapelekwa katika hifadhi ya maiti ya Lee, Nairobi.

Saa sita adhuhuri, mwili utapelekwa katika majengo ya Bunge kutoa nafasi kwa umma kuutazama na kutoa heshima zao hadi saa kumi na moja jioni.

Mnamo Ijumaa, kulingana Profesa Kindiki, mwili utapelekwa katika Uwanja wa Nyayo kwa ibada ya wafu itakayohudhuriwa na wageni mashuhuri kutoka nchini na ng’ambo.

“Baada ya hapo mwili utarejeshwa hifadhi ya Lee.” Akasema.

Mnamo Jumamosi, Oktoba 18, mwili utasafirishwa hadi Kisumu ambapo utawekwa katika Uwanja wa Michezo wa Moi, kutoa nafasi kwa umma kutoka heshima zao hadi saa kumi na moja jioni.

“Kisha utasafirishwa kwa barabara hadi nyumbani kwake Opoda Farm ambako utakaa huko usiku wote. Hatimaye mazishi yatafanywa Jumapili kulingana na taratibu za Kanisa la Kianglikana Nchini (ACK),” Profesa Kindiki akaeleza.