Habari za Kitaifa

Ijumaa ni Siku kuu ya kukumbuka Raila, serikali yatangaza

Na CHARLES WASONGA  October 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

SERIKALI imetangaza Ijumaa, Oktoba 17, 2025 kuwa siku ya pamuziko kwa heshima ya Hayati Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga aliyefariki mnamo Oktoba 15, 2025 akipokea matibabu katika hospitali moja nchini India.

Kupitia  gazeti maalum la serikali Waziri wa Usalama  Kipchumba Murkomen alitoa tangazo hilo kwa misingi ya Sehemu 3 ya Sheria kuhusu Sikuu za Kitaifa (Sura ya 110).

“Umma unajulishwa kwamba kwa misingi ya mamlaka inayotokana na Sehemu ya 3 ya Sheria kuhusu Sikuu za Kitaifa Waziri wa Usalama wa Ndani na Utawala wa Kitaifa ametangaza Ijumaa kuwa siku ya mapumziko kwa heshima ya Hayati Raila Odinga,” ikasema notisi hiyo.

Kulingana na ratiba iliyotolewa na Kamati ya Kitaifa ya Mazishi ya Kitaifa ya Raila, ibada ya wafu itafanyika siku hiyo Ijumaa Oktoba 17, 2025.

Kamati hiyo inayoongozwa na Naibu Rais Kithure Kindiki na Seneta wa Siaya Oburu Oginga ilitangaza kuwa mazishi ya mwenda zake yatafanyika Jumapili Oktoba 19, 2025 nyumba kwake Bondo, kaunti ya Siaya.