Oburu ateuliwa kiongozi mpya wa ODM
Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kimechagua Seneta wa Siaya, Oburu Odinga, kuwa kaimu kiongozi wa chama baada ya kifo cha kaka yake Raila Odinga.
“Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) ilikutana asubuhi hii na kwa pamoja ilikubaliana kumteua Seneta wa Kaunti ya Siaya, Dkt Oburu Odinga, kuwa kaimu kiongozi wa chama.Uteuzi huu unaanza mara moja,” taarifa ya ODM ilisema.
Baada ya mkutano huo, Gavana wa Mombasa Abdulswamad Nassir pia alifichua kwamba chama kimefungua vitabu vya rambirambi katika ofisi zake zote nchini, ambapo wananchi wanaweza kuandika jumbe za kuenzi kiongozi wao aliyefariki.
Alipendekeza pia wananchi wajitokeze kutazama mwili wa Raila, ambao utalazwa katika majengo ya Bunge kuanzia saa sita mchana hadi saa kumi na moja jioni.
Alisisitiza kwamba, licha ya kifo cha mwanzilishi na kiongozi wake kwa miongo miwili, chama kitaendelea kuwa imara katika jukumu lake.
“ODM inaendelea kama ilivyokuwa wakati wa Mheshimiwa Raila Amolo Odinga. Tunaamini katika umoja wa kusudi, chama thabiti cha kidemokrasia na chama kitakachoishi kwa miaka mingi ijayo,” alisema Gavana Nassir.
“Kwa hivyo, NEC imechagua Seneta wa Kaunti ya Siaya, Mheshimiwa Dkt Oburu Odinga, kuwa kiongozi wa muda wa chama, hadi wakati kamati kuu za chama zitakapokutana kumchagua kiongozi anayefaa kuchukua nafasi iliyoachwa na kiongozi wetu.”