Habari

Oburu atangaza mabadiliko hafla za kuaga Raila

Na CHARLES WASONGA October 16th, 2025 Kusoma ni dakika: 1

KAKAKE Hayati Raila Odinga, Oburu Oginga, ametangaza mabadiliko machache kuhusu ratiba ya umma kuutazama mwili wake na ibada ya wafu kwa heshima zake.

Akiongea na wanahabari nyumba kwa Raila, Opoda Farm, Bondo, Siaya, Dkt Oginga alisema kuwa ibada ya wafu itafanyika katika uwanja wa michezo wa Moi Sports Centre Kasarani badala ya uwanja wa Nyayo ilivyotangazwa Jumatano.

Aliongeza kuwa shughuli ya kutazama mjini Kisumu itafanyika katika Uwanja wa Michezo wa Jomo Kenyatta ulioko mtaani Mamboleo badala ya Uwanja wa Michezo wa Moi.

“Kulingana na msongamano wa waombolezaji ulioshuhudiwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Jomo Kenyatta (JKIA), tumeamua kuhamisha ibada yake ya wafu kutoka uwanja wa Nyayo hadi Kasarani, siku ya Ijumaa. Na mjini Kisumu siku ya Jumamosi, tumekubaliana kwamba mwili wake utatazwa katika uwanja wa Jomo Kenyatta, Mamboleo badala ya uwanja wa Moi ambao ni mdogo,”  Dkt Oginga akaeleza, ambaye ni mwenyekiti mwenza wa Kamati ya Kitaifa ya Kuandaa Mazishi ya Kitaifa ya mwendazake.

Seneta huyo wa Siaya alisema hayo Alhamisi alipofika Bondo kutoa habari rasmi kuhusu kifo cha Raila, kitendo kinachojulikana kwa dholuo kama “tero ywak pacho”.

Dkt Oginga pia alijumuisha na viongozi wa kidini kutambua sehemu ambako palichimbwa kaburi la Raila.

Seneta huyo wa Siaya aliandamana na viongozi wa Kanisa la Kianglikana (ACK) Dayosisi ya Bondo.

Raila atazimwa mita chache kando la kaburi la babake, Jaramogi Oginga Odinga, nyumbani kwao, Kango Kajaramogi, kijiji cha Nyamira.

Mnamo Alhamisi, mwili wa Raila ulitazamwa  na umma katika uwanja wa Kasarani; shughuli ambayo pia ilihamishwa kutoka majengo ya bunge kutokana na idadi kubwa ya waombolezaji.