Jaribio la mwisho la kumuokoa Raila kabla ya kufariki lafichuliwa
FAMILIA ya aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, pamoja na daktari bingwa wa moyo aliyemhudumia katika hospitali moja nchini India, wameeleza kwa uchungu juhudi za mwisho za kumuokoa kiongozi huyo mkongwe wa upinzani.
Wakenya walipokuwa wakijiandaa kwenda kazini alfajiri ya Jumatano, Hospitali ya Devamatha iliyoko Kerala, Kusini mwa India, ilikuwa kwa taharuki.
Bw Odinga alikuwa amepelekwa hospitalini humo kwa dharura baada ya kupata mshtuko wa moyo alipokuwa akitembea asubuhi saa mbili na nusu (saa kumi na mbili asubuhi saa za Kenya).
Aliandamana na daktari wake binafsi na mlinzi wake, Maurice Ogeta, ambao walijaribu kumpatia huduma ya dharura ya CPR. Bw Odinga hakurudiwa na fahamu, jambo lililowalazimu kumkimbiza hospitali iliyokuwa karibu zaidi.
Afisa wa polisi nchini India aliambia shirika la habari la AFP kuwa Bw Odinga alikuwa ameandamana na dada yake Ruth, binti yake Winnie, daktari wake binafsi na maafisa wa usalama wa Kenya na India.
Madaktari walichukua usukani wa juhudi za kuokoa maisha mara moja alipowasili.
“Hakuwa na mapigo ya moyo wala shinikizo la damu lililoweza kupimika alipowasili,” alisema Dkt Alphônš, bingwa wa moyo.