Wazee waidhinisha uteuzi wa Oburu Oginga kuongoza ODM
WAZEE kutoka Siaya wamempongeza Dkt Oburu Oginga kwa kuteuliwa kuwa Kaimu Kiongozi wa ODM, wakitaja uamuzi huo kuwa bora zaidi kwa chama hicho.
Mnamo Alhamisi, chama cha ODM kiliamua kumteua Dkt Oginga, kuwa kiongozi wa muda wa chama ili kuongoza maombolezi na kipindi cha mpito. Uamuzi huo ulitangazwa na Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) jijini Nairobi.
Wazee hao wanasema kuwa Dkt Oginga ndiye anastahili kusimamia chama katika kipindi hiki hadi kitakapochagua kiongozi rasmi, kutokana na uzoefu wake wa kisiasa na historia yake na Raila na ODM.
Mzee Onyango Radiel, ambaye amekuwa karibu na familia ya Odinga, asema kuwa Dkt Oginga amewahi kuwa mbunge katika Bunge la Taifa, Bunge la Afrika Mashariki na sasa Seneta wa Siaya hivyo ana tajriba faafu kuongoza ODM.
“Huu ni uamuzi bora kabisa. Kutokana na uzoefu huu mkubwa, tunaamini Oburu anaweza kutuongoza kama wanachama wa ODM,” alisema Mzee Radiel, aliyekuwa Mwenyekiti wa ODM tawi la Rarieda, Siaya.
Kulingana na wazee hao, kuna wengine waliofaa kuongoza chama kama Gavana wa Siaya, James Orengo, na Gavana wa Kisumu, Prof Anyang’ Nyong’o, ambao wamekuwa na Raila tangu zamani.
Walieleza kuwa hawa ni watu waliokuwa na imani na Raila, wana mawazo yaliyo sawa na yake, na wana uwezo wa kuongoza ODM.
“Tulikuwa na watu watatu akilini, Oburu, Orengo na Nyong’o. Wamekuwa na Raila kwenye mapambano. Chama kiko mikononi salama,” alisema Mzee Olang’o Nyabola.
Katika ibada ya wafu ya Raila katika uwanja wa Nyayo, Nairobi, Dkt Oginga alikubali wadhifa huo kwa unyenyekevu. Alisema kwamba licha ya kuwa kaka yake, alimtambua Raila kuwa kiongozi wake kisiasa.