Familia ya Raila yasifu Ruto, yataka Wakenya waendeleze maadili yake
FAMILIA ya marehemu aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga jana iliishukuru serikali ya Rais William Ruto kwa kugharimia matibabu yake India na kumpa mazishi ya kitaifa yenye taadhima kuu.
Wakiongozwa na kakake mkubwa Oburu Oginga na mjane Ida Odinga, watu wa familia hiyo pia walitoa wito kwa Wakenya kuendeleza maadili ambayo mpendwa wao alitetea na kupigania wakati wa uhai wake.
“Asante sana Rais William Ruto na serikali yako kwa kuingilia kati na kuhakikisha Raila anapata huduma za kimatibabu aliyohitaji,” Dkt Oginga akasema.
“Rais amesimama nasi tangu nilipomwambia kwamba ndugu yangu alikuwa mgonjwa, aliniambia nisiwe na wasiwasi. Alipanga usafiri na Raila akasafirishwa hadi India kwa matibabu,” Dkt Oburu akaeleza wakati wa ibada na mazishi ya Odinga iliyoandaliwa katika uwanja wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia ya Jaramogi Oginga Odinga (JOOSUT).
Dkt Oburu aliongeza kuwa Rais Ruto alifuatilia hali ya Raila hospitalini nchini India “hadi Mungu alipomchukua mnamo Jumatano ya Oktoba 15.”
“Kwa hivyo, kwa niaba ya familia ya Jaramogi Oginga Odinga, ninatoa wito kwa serikali na Wakenya kwa jumla kuendeleza juhudi za kutetea haki za kibinadamu, utawala bora unaozingatia katiba kama heshima kwa ndugu yangu,” akaeleza.
Kwa upande wake, Mama Ida, mjane wa marehemu Odinga, alitoa wito kwa uongozi wa kitaifa kutenda wema nyakati zote kwa heshima ya mwendazake.
Ida alimsifia mumewe na kuwataka wanasiasa kuendeleza uongozi bora na kutetea haki nyakati zote.
“Tafadhali tuzingatie haja ya kuleta mabadiliko nchini. Wanasiasa wakomeshe hulka ya kutaka kujilimbikizia utajiri bali wajali masilahi ya raia wanaokabiliwa na changamoto nyingi,” alisema.
Pia Mama Ida aliwashukuru watu wote waliosimama na familia yake wakati wa maombolezo.
Vilevile, alimtaja hasa Rais mstaafu Uhuru Kenyatta kwa kuwa rafiki wa kweli wa familia.
“Nataka kumtambua Rais mstaafu Uhuru Kenyatta. Yeye ni rafiki wa kweli. Alisimama kando yetu,” Ida alisema huku waombolezaji wakishangilia.
Na kwa mara ya kwanza, dadake Raila, Akinyi Wenwa, alionekana hadharani wakati wa ibada ya mazishi ya kakaye.
“Mimi ndimi Akinyi Wenwa yule ambaye mumekuwa mkimsikia. Watu humwita Raila ‘Wuodgi Akinyi’ yaani mimi hapa,” akasema akifichua kuwa yeye ndiye binti mkubwa wa Hayati Jaramogi Oginga Odinga.
Dkt Wenwa ni msomi na hajawahi kujitosa katika siasa. Kwa upande wake, Bi Ruth Odinga, ambaye ni Mbunge Mwakilishi wa Kisumu alimhakikishia Rais Ruto kwamba wao kama familia ya Odinga wataendelea kuunga mkono serikali yake.
“Isitoshe, chama chetu cha ODM kitasalia katika Serikali Jumuishi kuelekea uchaguzi mkuu ujao. Kwa hivyo, naomba wanachama wote kuwa waaminifu kwa serilkali hii,” akasema.
Watoto wa mwendazake Raila pia walipata fursa ya kuhutubia waombolezaji wakiongozwa na mtoto wake wa kiume, Raila Junior.
Wengine waliozungumza ni Rosemary Odinga na Winnie ambaye ni Mbunge katika Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA).
Winnie aliotoa dalili ya kuwania kiti cha kisiasa 2021 aliposema hivi: “Mheshima Rais ningetaka kukuhakikisha kuwa niko tayari kurudi nyumba.”