Ruto afunguka kwa mara ya kwanza kuhusu afya ya Raila kabla ya kifo chake
RAIS William Ruto Jumapili kwa mara ya kwanza alifunguka kuhusu matatizo ya kiafya yaliyomkumba aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga, miezi miwili kabla ya kifo chake Jumatano iliyopita.
Kiongozi wa nchi alifichua jinsi ambavyo familia ya Bw Odinga ilimpigia simu asubuhi siku ambayo alifariki India.
Akiongea wakati wa mazishi ya Raila Oktoba 19, 2025, Rais alisema kuwa ni Dkt Oburu Oginga alimfikia kwa mara ya kwanza kupitia ujumbe wa WhatsApp kuwa Raila alikuwa hali mahututi.

Ujumbe huo uliandikwa saa 12.45 asubuhi (saa moja kasoro robo) ya Jumatano.
Dkt Oburu alipiga simu dakika 10 baadaye na kumwaambia Rais kuwa inaonekana ‘tumempoteza Baba’.
Habari hizo zilithibitishwa kwa Rais Ruto na mwanawe Raila, Winnie Odinga, ambaye alikuwa naye India.
“Aliwapigia simu watu wengi akiwahakikishia kuwa yuko salama kiafya,” akasema rais bila kufichua maradhi ambayo yalikuwa yakimsumbua Raila.
“Mwezi moja uliopita ulikuwa mgumu sana. Sauti yake ilikuwa na mikwaruzo na alikuwa mnyonge kwa sababu alikuwa akitumia dawa na afya yake ilinishughulisha sana japo aliniambia alikuwa Dubai kupokea matibabu,” akasema Rais.
Alifunguka na kusema walifaa kukutana lakini mkutano huo haukufanyika kwa sababu madaktari wa Raila walikuwa wamemwaambia aende akapumzike kule Malindi, Kaunti ya Kilifi.
Raila aliporejea Nairobi kutoka Malindi alitaka kumwona Rais Ruto Ikulu lakini kiongozi wa nchi akahiari kuenda kwake mtaani Karen. Ni nyumbani kwa Raila ndiko waziri huyo mkuu wa zamani akamfahamisha kuhusu hali yake ya afya.
“Nilimwambia serikali itamlipia gharama ya matibabu kokote ambako angeenda iwe ni Amerika, Ujerumani, China ama India. Tulihakikisha kuwa tunashughulikia kila kitu alichotaka,” akaongeza Rais Ruto.
Vilevile Rais alifichua jinsi ambavyo ilikuwa vigumu kuongea na Winnie kuhusu kuharakikisha mazishi ya Raila ndani ya saa 72 alivyoandika katika wosia wake.