Habari za Kitaifa

Tofauti zaibuka ikiwa ODM itasalia ndani ya Serikali Jumuishi au la

Na CECIL ODONGO October 20th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

HATA kabla ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga kulazwa mchangani jana, tofauti zilidhihirika katika mazishi yake kuhusu iwapo chama kitasalia ndani ya Serikali Jumuishi au kitachukua mwelekeo mwingine wa kisiasa.

Katibu Mkuu wa ODM Edwin Sifuna alitofautiana na wenzake kuhusu suala hilo akionekana kutokuwa na imani kwamba ODM itaendelea kuunga mkono Serikali Jumuishi.

“Nani amewaambia kuwa ODM haitakuwa na mwaniaji wa urais 2027,” akasema Bw Sifuna akinukuu tamko la Raila mwenyewe mnamo Septemba 2022.

“Baba alikuwa anawasikia wananchi na nawaambia viongozi wa ODM tunyamaze tuwasikie wananchi wanataka tufanye nini,” akaongeza Bw Sifuna.

Hata hivyo, viongozi wengi waliohutubu walisisitiza kuwa ODM itasailia ndani ya Serikali Jumuishi.

“Siwezi kuwa mahali ambapo Raila hakunipelekea, nitaendelea kuheshimu siasa zake hadi hata kifo. Yeyote anayedhani kuwagawanya au kuvunja chama, wewe ndio utahama na chama kitakuwa hapa kudumu,” akasema Waziri wa Madini Hassan Joho.

Waziri wa Madini Opiyo Wandayi alisisitiza kuwa jamii ya Waluo wanaungana chini ya Dkt Oburu Oginga ambaye kwa sasa ni kaimu kiongozi wa ODM.

“Mimi na viongozi wengine tutahakikisha kuwa tunasalia ndani ya serikali hii ili watu wetu wanufaike. Raila amekufa kama tuko ndani ya serikali na hiyo ndiyo mwelekeo wetu, hakuna mwingine,” akasema Bw Wandayi.

“Nilikuwa naye mara ya mwisho na Seneta Eddy Oketch wa Migori ambapo alisema kuwa tusalie ndani ya Serikali Jumuishi. Kwa wale ambao wamebakia sote tuungane kuhakikisha kuwa chama kinakuwa imara na ndoto zake lazima zitimie,” akasema Waziri wa Vyama vya Ushirika na Biashara Ndogo ndogo Wycliffe Oparanya.

Kiongozi wa wachache Junet Mohamed alisema kuwa ODM mnamo 2027 haitakuwa kwenye muungano ambao ulikuwa ukimtusi Raila alipokuwa hai.

Alisisitiza kuwa chama hicho lazima kiunde serikali mnamo 2027 au kiwe kwenye muungano ambao utashinda uchaguzi.

“Alisema kuwa tukae ndani ya Serikali Jumuishi wale wana masikio wasikie na wale wenye macho waone,” akasema Bw Junet.

Gavana wa Siaya James Orengo naye alisema kuwa kitambulisho na thamani ya jamii ya Waluo ni chama cha ODM.

“Hii ODM ndiyo chama chetu kwa hivyo tufuate nyayo na demokrasia ambayo Raila alipigania wakati wa uhai wake. ODM ni chama ambacho kina msimamo na hilo lazima lidhihirike hata baada ya mauti ya Raila,” akasema Bw Orengo.

Viongozi wengine wa ODM ambao walisisitiza kuwa lazima ODM isalie serikalini ni mwenyekiti wa ODM Gladys Wanga, Dkt Oburu Oginga, Millie Odhiambo miongoni mwa viongozi wengine.

Bw Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki Babu Owino wamekuwa kati ya wanasiasa ambao wamekuwa waasi wa ODM wakipinga uwepo wa chama ndani ya Serikali Jumuishi.