Kifo cha Raila kinavyoweka nchi nzima njia panda kisiasa
KUFUATIA mauti ya aliyekuwa Waziri Mkuu na Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, wengi sasa wanasubiri kufahamu mwelekeo ambao siasa za nchi utachukua.
Kwa miaka mingi, siasa za nchi zimekuwa zikiegemea kwa Raila. Kuna wale ambao wamekuwa wakimpinga na kupata umaarufu kisha kushinda viti vya kisiasa.
Kwa upande mwingine, kuna wale ambao wamekuwa wakimuunga na kusubiri kuinuliwa mkono kisha kuwahi viti vya kisiasa kila mwaka wa uchaguzi.
Kitaifa, Raila amekuwa mwanasiasa ambaye aliteka wafuasi wake ambapo uamuzi wake umekuwa ukisubiriwa kila mara ambapo nchi ipo njiapanda kisiasa.
Kabla ya mauti yake, mwelekeo na kila hatua iliyokuwa ikichukuliwa na Raila, ilikuwa ikifuatwa na serikali na pia vinara wa upinzani.
Raila aliaga dunia akiwa ndani ya Serikali Jumuishi lakini vinara wa upinzani Kalonzo Musyoka na Rigathi Gachagua kando na kumvamia, bado walikuwa na matumaini ya kupata uungwaji mkono wake kuelekea kura ya 2027.
Raila aliondokea kujizolea sifa kama mwanasiasa ambaye alipambania mfumo wa vyama vingi nchini katika miaka ya 90 na pia Katiba Mpya inayotumika sasa ambayo ilizaa serikali za ugatuzi.
“Nawahakikishia wanachama wa ODM kuwa tutawaunga mkono kwa sababu Baba aliamini katika mfumo wa vyama vingi. Nguvu za ODM kwangu ni muhimu kwa sababu hivyo ndivyo tutakuwa na demokrasia komavu,” akasema Rais Ruto mnamo Jumapili wakati wa ibada ya mazishi ya Raila eneobunge la Bondo, Kaunti ya Siaya.
“ODM itabuni serikali ijayo au kuwa sehemu ya serikali ijayo. Kile ambacho sitakubali kwa heshima ya Odinga ni watu kuchezea ODM na kukiacha chama kwenye upinzani,” akasema Rais Ruto.
ODM kwa sasa imegawanyika huku mrengo mmoja ukiunga kuchaguliwa kwa Rais Ruto tena mnamo 2027 naye Katibu Mkuu Edwin Sifuna, anapinga utawala wa sasa.
Kiongozi wa wachache katika Bunge la Kitaifa Junet Mohamed naye alikiri kuwa ni kweli maisha ya wanasiasa wengi hayatakuwa rahisi kutokana na kuondoka kwa Raila.
“Nimewaona watu katika mtandao wa kijamii wakisema mimi sasa ni yatima. Lakini nikija hapa nimewaona mayatima wengi, na wengi wakilia,” akasema Bw Mohamed.
“Kwa hivyo, nitawakusanya mayatima hawa wote niwe mwenyekiti wao,” akaongeza Bw Mohamed huku akiibua ucheshi.
Wako hata waliokuwa wakitumia upinzani wao dhidi ya Raila kuchaguliwa hasa ukanda wa Mlima Kenya. Nao pia wamepoteza.
Wiki jana, Kamati Kuu ya Kitaifa ya ODM iliandaa na kumtangaza Dkt Oburu Oginga kuwa kaimu kiongozi wa chama.
Dkt Oginga ni mwandani wa Rais Ruto na wachanganuzi wa kisiasa wanasema itakuwa rahisi kwake kuunda ushirikiano kati ya ODM na UDA akiwa ameshikilia usukani.
“Kukosekana kwa Raila ghafla kumesababisha pengo la kisiasa na wengi bado wamechanganyikiwa,” akasema Mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Profesa Gitile Naituli.
Naibu Kiongozi wa Safina Willis Otieno ambaye alikuwa msimamizi wa kampeni za Raila mnamo 2017 naye anasema kuwa Rais William Ruto ndiye ameathirika sana kisiasa kutokana na kutokuwepo kwa Raila.
“Raila ndiye alifanya serikali ya Rais Ruto iwe na uthabiti baada ya maandamano ya Gen Z mwaka jana,” akasema Bw Otieno.
Kiongozi huyo anashikilia kuwa Bw Odinga ametawala anga za kisiasa nchini kwa zaidi ya miaka 30 na wengi wamejikuza kisiasa kwa kutumia jina lake na wengine kupinga siasa zake.