Habari za Kitaifa

Raila ageuzwa shujaa wa Mashujaa Dei akituzwa na kuenziwa kote

Na CHARLES WASONGA October 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 3

SHEREHE za Kitaifa ya Mashujaa Dei za mwaka huu zilizofanyika jana katika kaunti ya Kitui, zilitumika kumuenzi zaidi marehemu aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga aliyezikwa Jumapili.

Rais William Ruto aliyeongoza hafla hiyo katika uwanja wa michezo wa Ithookwe, mjini Kitui, alimtunuku Odinga tuzo ya kitaifa ya juu zaidi nchini ya “Chief of the Golden Heart of Kenya” (CGH).

Mtu wa hivi punde Rais Ruto kutunukiwa hadhi hiyo ni Muadhama Mwanamfalme Rahim Al-Hussaini Aga Khan V, mnamo Agosti 26, mwaka huu alipozuru Kenya.

Akihutubia taifa, Rais Ruto alisema tuzo hiyo inatambua mchango wa Raila wa kipekee katika kuboresha taifa hili na kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

“Serikali na raia wa Kenya wanaweka jina la Mheshimiwa Raila Odinga miongoni mwa mashujaa wetu wakuu, katika muhuri wa Jamhuri,” Rais Ruto akasema.

“Kwa niaba ya taifa hili kuu na kupitia mamlaka niliyopewa kama Rais, leo (jana) nimempa Mheshimiwa Raila Amolo Odinga, tuzo ya heshima kuu zaidi ya Jamhuri, “Chief of the Golden Heart of Kenya (CGH),” akasema.

Aidha, tangazo rasmi kuhusu tuzo hiyo liliwekwa katika Gazeti Rasmi la Serikali la Oktoba 20, 2025.

Tangazo hilo linaangazia mseto wa sifa za Odinga, tangu alipohudumu kama mhadhiri wa chuo kikuu, hatamu yake kama mbunge kwa miaka 20, huduma yake kama waziri hadi wajibu wake wa kihistoria kama Waziri Mkuu wa pili wa Kenya.

Pia linaangazia nafasi yake kama kiongozi mkuu serikalini na katika upinzani, kielelezo cha nafasi yake ya kipekee katika historia ya taifa hili.

“Katika maisha, iwe ndani ya serikali au nje, Mheshimiwa Raila Amolo Odinga ulionyesha ujasiri, uvumilivu, moyo wa kujitolea na utetezi wa demokrasia, utawala bora, utetezi wa maadili ya Afrika na huduma kwa wananchi wote,” linaeleza tangazo hilo la gazeti rasmi la serikali.

Jana katika uwanja wa Ithookwe, Rais Ruto, alikariri sifa hizo akieleza kuwa mchango wa Odinga katika ustawi wa taifa utakumbukwa na vizazi vingi vijavyo.

Kiongozi wa taifa alieleza kuwa mwendazake alielewa kuwa, dhima ya uongozi sio kujipatia makuu bali ni kuhudumia taifa na kuliweka thabiti.

“Raila aliipenda Kenya kwa moyo wake wote, kwa kujitolea na bila masharti. Wakati mmoja alisema kuwa angekuwa na Mungu amuulize alikotaka kuzaliwa tena, angesema bila kusita kuwa arejeshwe Kenya. Alifahamu kuwa Kenya, kama mataifa yote, haikukosa dosari zake,” Rais Ruto akasema.

Kiongozi wa taifa alisema marehemu Raila alielewa kuwa Kenya ilikuwa ni nchi inayoendelea na hilo halingefikiwa kwa muujiza.

“Odinga aliamini kuwa ilikuwa ni wajibu wake kujitolea mhanga kwa juhudi za kufikiwa kwa ndoto ya taifa hili,” Dkt Ruto akasema.

Alisema kuwa maishani mwake, marehemu Waziri Mkuu wa zamani alipenda kufanya maridhiano kwa manufaa ya nchi, licha ya uwepo wa migawanyiko ya kisiasa.

Rais Ruto aliwakumbusha Wakenya jinsi alimtafuta Raila wakati wa maandamano ya kupinga serikali yake mwaka jana, na akakubali kwamba waunde serikali jumuishi kwa manufaa ya taifa.

“Mashujaa hufanya hivi. Hatari inapotokea wao hujitokeza na kufanya yake yanayolinda uthabiti wa nchi bali sio ya manufaa yao binafsi. Hata baada ya uchaguzi mkuu uliopita tulipotengana Baba aliweka mbele maslahi ya nchi,” Dkt Ruto akaeleza.

Kiongozi wa taifa alisema kuwa marehemu aliyekuwa kiongozi wa chama cha ODM, hakuwa na uchu mkubwa wa kuwa rais, lakini haja yake kuu ilikuwa ni kuhakikisha kuwa Kenya inakuwa na rais atakayeisongeza nchi mbele kimaendeleo.

“Hii ndio maana kuelekea uchaguzi mkuu wa 2022 alisema Kibaki Tosha, kwa manufaa ya taifa hili,” Dkt Ruto akasema.

Mgeni mheshimiwa katika sherehe za Mashujaa Dei za mwaka huu, Rais wa Senegal Bassirou Diomaye Faye alihimiza kuwa mashujaa wa Kenya waendelee kukumbukwa kwa mchango wao kwa uhuru wa Kenya.

Rais huyo pia aliwasilisha rambirambi kwa familia na taifa la Kenya kwa ujumla akimtaja Odinga kama kiongozi aliyetoa mchango mkubwa zaidi katika ulingo wa siasa nchini humu.

Mgeni mwingine aliyehudhuria sherehe hizo ni Waziri Mkuu wa Msumbiji Bi Maria Benvinda Levy.

Nyimbo zilizowasilishwa kutoa burudani kwa waliohudhuria sherehe hizo pia zilisheheni maudhui ya kumuezi Hayati Rail Odinga.