Habari za Kitaifa

Rais Ruto aachia Ukambani miradi tele ya mabilioni

Na KITAVI MUTUA October 21st, 2025 Kusoma ni dakika: 1

RAIS William Ruto jana aliachia Kaunti ya Kitui na ukanda mzima wa Ukambani miradi si haba baada ya kuongoza sherehe ya Mashujaa Dei.

Miradi hiyo ilikuwa katika sekta za barabara, maji, kawi na nyumba pamoja na ahadi tele kukamilishwa kwa ile iliyoanzishwa.

Aliahidi kurejea eneo hilo baada ya wiki mbili kuzindua miradi hiyo.

Rais awali alikuwa ameratibiwa kutembelea eneo hilo kwa siku tano lakini akaahirisha ziara hiyo kufuatia kifo cha Raila Odinga.

Alitangaza kuwa kuna miradi minne mikubwa ya barabara inayogharimu mabilioni ya pesa itatekelezwa Kitui, kisha mingine miwili Machakos na Kitui.

Serikali pia inaendeleza ujenzi wa masoko nane ya kisasa katika maeneobunge yote manane ya Kaunti ya Kitui.

Uga ulioandaa sherehe za jana wa Ithookwe ulijengwa ndani ya miezi minne kwa kima cha Sh800 milioni.

Pia alitangaza kuwa bwawa la High Grands Falls ambalo litakuwa la pili kwa ukubwa Afrika, litajengwa Ukambani kwenye mpaka wa kaunti za Kitui na Tharaka-Nithi.