Mamia bado hospitalini baada ya mkanyagano wakati wa utazamaji mwili wa Raila
MAMIA ya watu bado wamelazwa Hospitali ya Kenyatta (KNH) kutokana na mkanyagano uliozingira kutazamwa kwa mwili wa aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga jijini Nairobi na Kisumu wiki jana.
Mikanyagano hiyo ilitokea Oktoba 16, 17, 19 katika majengo ya Bunge na pia katika viwanja vya MISC Kasarani, Nyayo na Jomo Kenyatta, Mamboleo, Kisumu.
Mbali na majeraha, kumeripotiwa pia visa mbalimbali vya mauti.
Mkurugenzi wa Shirika la Vocal Afrika Hussein Khalid alieleza Taifa Leo kuwa kulikuwa na zaidi ya vifo saba Nairobi huku KNH ikilemewa kutokana na idadi ya juu ya majeruhi.
Seneta wa Busia Okiya Omtata kwenye mtandao wake wa X alisema alitembelea KNH na kusema madaktari wamelemewa na idadi ya juu ya wale ambao walijeruhiwa katika hafla za makaribisho na ibada ya kumuenzi Raila.
Afisa Mkuu Mtendaji wa KNH Richard Lesiyampe wiki jana alisema walipokea majeruhi 34 na akasema hawawezi kuwatibu bure.