Wakazi wafurahia ukarabati wa barabara ya zamani ya Kitengela–Namanga
Mamia ya watumiaji wa barabara ya zamani ya Kitengela–Namanga wamepata afueni baada ya Mamlaka ya Barabara za Mijini (KURA) kutangaza kutenga imetenga Sh100 milioni zaidi kwa ukarabati wa barabara hiyo.
Fedha hizo zitatumika kujenga kilomita mbili zaidi, kuongezea kilomita mbili za awali zilizokarabatiwa kwenye barabara ya kilomita tisa inayoanzia mjini Kitengela, kupitia maeneo ya makazi, hadi kuungana na barabara kuu ya Namanga nyuma ya shamba la maua la Masai Flowers.
Ukarabati huo unakuja baada ya kilio cha muda mrefu kutoka kwa wakazi waliokuwa wakihangaika kutokana na hali mbaya ya barabara hiyo, ambayo wanasema ni muhimu kwa uchumi wao.
Awali, KURA ilikuwa imetenga Sh 64 milioni kuweka lami kilomita moja na kutengeneza sehemu iliyosalia mnamo Machi 2024. Miezi kadhaa baadaye, fedha zaidi zilitolewa kwa kilomita nyingine, hatua iliyowapa matumaini mapya wakazi.
Fedha za sasa zilizotangazwa wiki jana zinatarajiwa kuongeza lami hadi kituo cha polisi cha Milimani, hivyo kupunguza gharama ya usafiri kwa wakazi wa eneo hilo.
“Hii ni hatua nzuri. Tunaomba serikali itenge fedha zaidi ili barabara hii yote ikarabatiwe. Tumeteseka kwa miaka mingi,” alisema mkazi Gerald Kimani.
Mbunge wa Kajiado Mashariki, Bw Kakuta Mai Mai alisema mkandarasi ataanza kazi mara moja kwani mradi huo umesubiriwa kwa muda mrefu. Aliongeza kuwa vijana wa eneo hilo watapewa ajira za vibarua katika mradi huo.
“Ujenzi wa barabara hii ulicheleweshwa sana. Tumefanya ushawishi mkubwa. Kukamilika kwake kutafungua uchumi wa eneo hili na kupunguza msongamano kwenye barabara ya Namanga. Hii ni hazina kwa wakazi wa Kitengela,” alisema Bw Mai Mai.