Raila: Kwa nini wakazi wa Kondele bado hawaamini hayuko
WAKAZI wa mtaa wa Kondele, mjini Kisumu, wanajulikana kwa ufuasi na uaminifu wao kwa aliyekuwa kiongozi wa ODM Raila Odinga.
Hata baada ya kifo chake, wakazi hao walikesha kuanzia siku hiyo, Jumatano Oktoba 15, hadi alipozikwa Jumapili, Oktoba 19, 2025.
Siku kadhaa baada ya mazishi ya Odinga, wengi wa wakazi wa Kondele bado hawaamini kuwa hawatamwona tena.
Tulipotembelea mtaa huo Jumanne, Oktoba 21, 2025, wakazi waliketi kwa makundi wakipiga gumzo kuhusu marehemu mwanasiasa huyo mkongwe.
Baadhi yao walikubali kwamba maisha hayarejelei kawaida huku wakiendelea kumwomboleza Bw Odinga huku wengine waliungama kuwa hayuko na kuahidi kuendeleza maadili yake.
Kwao, Bw Odinga hakuwa tu kiongozi wa kisiasa, alikuwa mwelekezi wao na aliyewapa matumaini kuhusu mazuri ya kesho. Ni mtu wa kipekee waliyetii amri yake pasina kuuliza swali lolote.
Wakazi wanaamini Kondele ilikuwa “ngome ya kisiasa” ya Bw Odinga na pia ilijulikana kama “Barracks” (kambi ya jeshi).
Ni katika mtaa wa Kondele na ule wa Kibra, Nairobi ambako wafuasi wa Bw Odinga wangefanya maandamano kudhihirisha hasira au furaha yao, kulingana na upande ambako mwanasiasa huyo alikuwa akiegemea.
“Katika utekelezaji wa maagizo ya Bw Odinga, tulikuwa mstari wa mbele. Kile tulihitaji ni yeye kuongea na tungetenda,” anasema Bw Jose Owino, mkazi wa Kondele.
Kwake, habari za kifo cha Odinga bado zinaonekana kama ndoto mbaya ambayo anataka imwondokee.
Mkazi huyo wa Kondele anasema kuwa amekuwa mfuasi sugu wa Bw Odinga tangu 1997 alipowania urais na kumaliza namba tatu kwa tiketi ya chama cha National Development Party (NDP).
Tangu wakati huo, Owino amesalia mwaminifu kwa mwanasiasa huyo hadi alipokufa alipokuwa akipokea matibabu nchini India mnamo Oktoba 15, 2025.
“Wakati huo, nilikuwa kijana na nilikuwa nimejisajili kuwa mpiga kura. Alipogura chama cha babake cha Ford Kenya na kujiunga na NDP, nilikuwa tayari kumuunga mkono,” anasema Owino.
Anaeleza kuwa alimuunga mkono Odinga kwa miaka kadhaa kutokana na hali kwamba alimpenda babake, Hayati Jaramogi Oginga Odinga.
Kwa Bw Owino, Jaramogi alidhihirisha sifa bora za uongozi, na bila shaka aliamini kuwa mwanawe angefuatia mfano wake.
“Hata baada ya Raila kujiunga na chama cha Kanu na muungano wa Narc miongoni mwa vyama vingine hakuwahi kumpinga,” akasema Owino anayeonekana mwenye majonzi.
Kwa upande wake, Nicholas Owino, mkazi mwingine wa Kondele alisema Odinga alichangia pakubwa kukamilishwa kwa ujenzi wa daraja la juu kwa juu la Kondele Fly Over miongoni mwa miradi mingine muhimu mjini Kisumu.
Hii ndio maana aliamua kusafiri hadi Bondo, kaunti ya Siaya kutoa heshima zake za mwisho mwa mwendazake.
Wafuasi hao walikuwa na matumaini kwamba msafara wa kusafirisha mwili wake ungepita Kondele kutoka uwanja wa ndege wa kimataifa wa Kisumu lakini mioyo yao ilivunjika mipango ilipobadilishwa na mwili ukasafirishwa kwa helikopta ya kijeshi hadi katika uwanja wa Mamboleo.