‘Mayatima wa Raila’ walumbania chama hata kabla ya kaburi kukauka
MGAWANYIKO wa kisiasa ndani ya Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) umeibua mjadala mkubwa kuhusu hatima ya chama hicho kufuatia kifo cha kiongozi wake, Raila Odinga, aliyezikwa Jumapili iliyopita.
Bw Odinga alikuwa nguzo ya chama hicho, akihudumu kama mpatanishi mkuu kati ya wanachama na kuzuia migogoro kila ilipozuka.
Uwezo wake wa kuleta mshikamano na kusuluhisha migogoro umefanya wengi kumuona kama gundi ya chama, na sasa ODM inakabiliwa na changamoto kubwa ya kuendelea bila yeye.
Baada ya kifo chake, Kamati Kuu ya Taifa ya ODM ilimteua kakake Raila, seneta wa Siaya, Oburu Oginga, kuwa kaimu kiongozi wa chama.
Katika ibada ya wafu iliyofanyika Uwanja wa Nyayo, Jumatano, Dkt Oginga alikiri changamoto kubwa iliyopo mbele ya chama na kuahidi kujaribu kuendeleza malengo aliyokuwa nayo ndugu yake Raila.
Hata hivyo, chama kinakumbwa na migogoro ya ndani inayotokana na ushirikiano na serikali ya Rais William Ruto.
Katibu Mkuu Edwin Sifuna, ameonyesha kutoridhishwa na mpango huu na yeye na viongozi vijana wanahisi chama kinapaswa kuacha ukuruba wa sasa na serikali na kukumbatia upinzani.
Hali hii imesababisha migawanyiko mikubwa ndani ya ODM.
Mgawanyiko wa kizazi ndani ya chama unaongeza msukosuko. Kundi la Bw Sifuna na Mbunge wa Embakasi Mashariki, Babu Owino, linatofautiana na wanachama wakongwe kama James Orengo, Anyang’ Nyong’o na Oburu Oginga huku wachanganuzi wakisema tofauti hizi zinaweza kuharibu chama ikiwa hazitashughulikiwa vyema.
Swala jingine muhimu ni mkondo wa chama kuelekea uchaguzi mkuu wa 2027. Makundi mawili yamejitokeza ndani ya ODM, kila moja likitaka njia tofauti.
Kundi moja linajumuisha mwenyekiti wa chama Gladys Wanga, mawaziri wanne walioko serikalini, na naibu kiongozi Abdulswamad Nassir.
Wana msimamo thabiti wa kuendelea kushiriki katika serikali jumuishi, sasa na baadaye.
Wanaamini ushirikiano huu unaleta manufaa ya kisiasa na kiuchumi kwa chama na wanajitahidi kuendeleza ushawishi ndani ya serikali.
Wakati huo huo, kundi la Bw Sifuna linashikilia msimamo kuwa chama kinapaswa kuwa upande wa upinzani na kujiandaa kuwania urais kupitia mgombeaji wa ODM mwenyewe.
Katika mazishi ya Raila, Waziri wa Fedha John Mbadi na Waziri wa Madini Hassan Joho waliwahakikishia wanachama kuwa watabaki katika serikali chini ya Rais Ruto, jambo linaloashiria mgawanyiko zaidi.
Waziri wa Kawi Opiyo Wandayi, alisema, “Baba Raila Amolo Odinga alituachia serikali ya Rais William Ruto, na ndipo tutakapoendelea kuwa hadi mwisho.”
Hali hii inaonyesha kuwa msimamo wa chama bado haujakuwa mmoja.
Bw Mbadi aliongeza: “Raila alitufundisha kuwa tunapaswa kuwa katika serikali kama jamii, na kama chama tutamuunga mkono Rais Ruto na serikali yake.”
Bw Mbadi alisema chama kitatoa mwelekeo kamili ndani ya siku 30 zijazo kuhusu msimamo wake kisiasa.
Katika mahojiano na gazeti la Taifa Leo, Mbadi alisema kuwa kiongozi mpya wa chama atatokea kwa njia ya kawaida kwa mujibu wa mahitaji ya jamii.
Aliongeza kuwa Raila alijijenga kisiasa baada ya kifo cha baba yake mnamo 1994 na kuwa msemaji wa jamii kwa sababu ya msimamo wake thabiti na juhudi za kuleta maendeleo.
“Mabadiliko haya yatajiri kwa njia asili. Inahitaji mtu kupigania haki za jamii na kuonyesha atakavyoisaidia,” alisema.