Afisi ya Kindiki yatumia karibu nusu ya bajeti ya 2025/2026 ndani ya miezi minne
AFISI ya Naibu Rais Kithure Kindiki imefyonza karibu nusu ya bajeti yake ya matumizi, ndani ya robo ya kwanza ya mwaka huu wa kifedha.
Hayo yanafichuka wakati shughuli za kisiasa zimeongezeka kote nchini, haswa michango ya kuyawezesha makundi mbalimbali ambayo Profesa Kindiki amekuwa akiongoza katika miezi kadhaa iliyopita.
Kulingana na data iliyochapishwa na Hazina ya Kitaifa, Afisi ya Naibu Rais ilikuwa imetumia Sh1.34 bilioni kufikia Septemba 30, 2025, kiasi ambacho ni sawa na asilimia 44.9 ya bajeti yake ya Sh2.97 bilioni ambayo ndio bajeti yake ya matumizi ya kawaida katika mwaka wa Kifedha wa 2025-2026.
Kwa hivyo, afisi hiyo imesalia na Sh1.63 bilioni za matumizi katika miezi tisa iliyosalia kabla ya mwaka huu wa kifedha kutamatika Juni 30, 2026.
Hii ina maana kuwa, afisi hii ni miongoni mwa asasi za serikali zinazotumia kiasi kikubwa cha pesa kwa shughuli za kawaida.
Ikiwa itadumisha kasi hii ya matumizi ya fedha, ikitimu Machi 2026, afisi hiyo itakuwa imemaliza mgao wake. Halii hii italazimu afisi hiyo kutengewa pesa zaidi kupitia bajeti ya ziada.
Rekodi za Hazina Kuu zinaonyesha kuwa, kasi ya matumizi ya pesa katika Afisi ya Profesa Kindiki imezidi, mara nne, ile ya mtangulizi wake Rigathi Gachagua.
Kwa mfano, kufikia Septemba 2024, afisi hiyo chini ya Gachagua ilikuwa imetumia Sh331.8 milioni, sawa na asilimia 12.8 ya mgao wa kila mwaka wa bajeti ya matumizi ya kawaida, wakati huo.
Bajeti hiyo inajumuisha pesa za kulipa mishahara ya wafanyakazi, marupurupu, usafiri, uendeshaji afisi, gharama ya ukarabati na ushirikishi wa mipango ya serikali chini ya Afisi ya Naibu Rais.
Profesa Kindiki, ambaye aliingia afisini Novemba 1, 2024 baada ya kutimuliwa kwa Gachagua mnamo Oktoba 18, mwaka huu, katika siku za hivi karibuni amekuwa akiongoza msururu wa michango ya kuwawezesha makundi ya boda boda, akina mama na vijana.