Habari za Kitaifa

Kahiga motoni kwa ‘kusherehekea’ kifo cha Raila

Na BENSON MATHEKA October 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Kauli ya gavana wa Kaunti ya Nyeri, Mutahi Kahiga, aliyoonekana kusherehekea kifo cha aliyekuwa waziri mkuu hayati Raila Odinga zimemwingiza kwenye moto viongozi kadhaa na Wakenya wakimkosoa vikali kwa kukosa utu.

Hii ni baada ya video iliyosambaa mitandaoni  akitoa kauli zinazoonekana kuhusisha kifo cha Raila Odinga na “mpango wa Mungu” kwa faida ya eneo la Mlima Kenya ambayo imekera viongozi wengi wakimtaka atoe maelezo ya wazi na  kwa baadhi yao wakimtaka aombe msamaha.

Akizungumza katika hafla ya mazishi eneo la Nyeri mnamo Oktoba 21, 2025, Kahiga alisema kwa Kikuyu:

“Mmekiona kile kilichokuwa kimeandaliwa, lakini Mungu alileta jambo. Sasa ni mchanganyiko kamili. Hatukuwa na chuki kwa mtu yeyote, lakini Mungu alitokea kwa ajili yetu.”

Kauli hizi ziliwachemsha viongozi na wananchi kutoka mirengo yote ya kisiasa. Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kupitia taarifa kilimtaka gavana Kahiga “aombe msamaha” kwa kauli zake.

“Haya ni maneno yasiyofaa kwa wakati huu wa maombolezo ya kiongozi wetu Raila Odinga,” ilisema taarifa ya ODM.

Viongozi wa eneo la Mlima Kenya wakiongozwa na gavana  Anne Waiguru wa Kirinyaga walimkemea vikali Dkt Kahiga kwa kauli alizotaja kama “zisizo na heshima, mbaya na za kuzua tofauti za kikabila”.

Baraza la magavana (CoG) ambalo Dkt Kahiga ni naibu mwenyekiti pia lilijitenga  na kauli hizo zilizotaja kama “hatari kwa mshikamano wa kitaifa”, huku baadhi ya Wakenya wakihimiza avuliwe wadhifa wake katika baraza hilo.
Mwenyekiti wake, Ahmed Abdullahi, alisema kauli hiyo haionyeshi maadili ya uongozi wala heshima kwa kiongozi aliyefariki na akaita kikao cha wenzake Oktoba 22 2025 kumjadili Kahiga.

Seneta wa Nandi, Samson Cherargei, alimshambulia Kahiga kwa “kusherehekea kifo kwa faida yake” na kusema maneno hayo ni “kinyume kabisa cha utamaduni wetu wa Waafrika.”

Raila Odinga alikufa Oktoba 15, 2025 akitibiwa nchini India akiwa na umri wa miaka 80 na kuzikwa Jumapili iliyopita katika kijiji cha Nyamira, Bondo kaunti ya Siaya.

Seneta wa Narok  Ledama Olekina ameahidi kuchukua hatua kali dhidi ya Gavana Kahiga baada ya kauli zake zinazoonekana kusherehekea kifo cha Raila.

Katika video iliyosambaa mitandaoni, Kahiga anaonekana akihutubia waombolezaji kwa lugha ya Kikuyu, akidai kuwa kifo cha Raila Odinga kitaleta maendeleo katika ukanda wa Kati wa Kenya. Gavana huyo alisema kuwa kiongozi wa chama cha Orange Democratic Movement (ODM) aliyeaga dunia alikuwa chanzo cha eneo hilo kusahaulika kimaendeleo na serikali ya kitaifa.

Jaji Mkuu Mstaafu David Maraga, amelaani kauli hizo akinukuu  Ibara 73 (1) ya Katiba ya Kenya ya 2010.
“Kauli za Gavana Kahiga kuhusu kifo cha Raila Odinga zinakiuka katiba,” alisema Maraga..