Habari za Kitaifa

Watoto 75 wazaliwa siku moja Kitengela, idadi ya vifo vya wajawazito ikipungua

Na STANLEY NGOTHO October 22nd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Mnamo Jumatatu, Oktoba 20, 2025, watoto 75 walizaliwa katika Hospitali ya Kitengela Level 4 ndani ya saa 24, jambo linaloashiria ongezeko kubwa la akina mama wajawazito wanaotafuta huduma salama za kujifungua katika Kaunti ya Kajiado.

Katika kipindi cha miezi sita iliyopita, idadi ya wanawake wajawazito wanaotafuta huduma za uzazi imeongezeka mara tatu, hatua iliyosaidia kupunguza kwa kiwango kikubwa vifo vya kina mama wakati wa kujifungua.

Hospitali hiyo, ambayo hivi majuzi ilipandishwa hadhi kuwa ya Level 4, inahudumia wakazi wa mji wa Kitengela unaokua kwa kasi na maeneo jirani ikiwemo wakazi wa Athi River na Mlolongo katika Kaunti ya Machakos.

Aidha, wodi ya uzazi inahudumia mamia ya wakimbizi wanaoishi katika mji  wa Kitengela chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa (UN).

Mkunga Mkuu wa Hospitali hiyo, Dkt Veronica Abuto, aliambia Taifa Leo siku ya Jumanne kwamba hospitali hiyo ilishuhudia idadi ya juu kabisa ya watoto kuzaliwa katika historia yake, siku ya Mashujaa.

Kulingana na takwimu, jumla ya watoto 75 walizaliwa huku wanawake 68 wakijifungua ndani ya saa 24, ambapo wanawake saba walijifungua mapacha. Kati ya hao 68, wanawake 25 walijifungua kwa njia ya upasuaji huku 43 wakijifungua kawaida. Jumla ya vifo vitano vya kina mama na watoto wachanga vilirekodiwa.

“Hospitali yetu kwa sasa imelemewa na idadi kubwa ya wanawake wanaotafuta kujifungua salama. Ni sera yetu kutowakataa wajawazito wanaohitaji huduma. Katika miezi sita iliyopita, tumeweza kupunguza pengo la vifo vya kina mama,” alisema Dkt Abuto.

Takwimu zinaonyesha kwamba mwezi Septemba 2025, kulikuwa na jumla ya watoto 466 waliozaliwa, kati yao 312 walizaliwa kawaida na 154 kwa njia ya upasuaji. Watoto 15 walifariki, akiwemo waliokufa tumboni. Mwezi Agosti, kulikuwa na watoto 479 waliozaliwa, ambapo 119 walizaliwa kwa upasuaji na vifo 11 vya watoto wachanga viliripotiwa.

Mnamo Julai 2025, kati ya watoto 364 waliozaliwa, 254 walizaliwa kawaida na 110 walizaliwa kwa upasuaji. Angalau watoto wachanga saba walifariki dunia.

Idara ya uzazi ya hospitali hiyo imekuwa ikifanya wastani wa kujifungua  watoto 500 kila mwezi, ambapo takriban 400 huzaliwa kawaida na karibu 100 kwa njia ya upasuaji.

Mmoja wa wakimbizi kutoka Congo aliye nchini chini ya mpango wa Umoja wa Mataifa alisema hospitali hiyo imekuwa “kimbilio salama” kwa wanawake wakimbizi kutoka Rwanda na Congo. Kauli hii iliungwa mkono na akina mama wapya waliohojiwa na Taifa Leo.

“Tunakuja hapa kwa ajili ya kujifungua kwa usalama. Bila matatizo yoyote, mtu huondoka ndani ya saa 24,” alisema mama huyo huku akiwa amemshika mtoto wake wa kwanza wa kiume.

Ili kukidhi mahitaji ya wingi wa wajawazito wanaofika kila siku, idara ya afya ya kaunti imezindua jumba jipya la upasuaji kushughulikia dharura wakati wa kujifungua.

Waziri wa Afya wa Kaunti Bw Alex Kilowua alisema jumba hilo jipya litakuwa nguzo muhimu katika juhudi za kupunguza vifo vya akina mama wakati wa kujifungua hadi kufikia sifuri katika mji huo wenye idadi kubwa ya watu. Alisema jumba hilo la kisasa limewekwa vifaa na madaktari wameajiriwa.

“Tumetenga jumba hili jipya kwa ajili ya upasuaji wakati wa kujifungua na dharura nyingine za kujifungua,” alisema Kilowua wakati wa uzinduzi rasmi Jumanne.