Serikali yawapa matumaini wawekezaji wa Ekeza
Na MWANGI MUIRURI
SERIKALI imelegeza masharti ya utendakazi dhidi ya kampuni ya akiba na mikopo ya Ekeza na ambayo humilikiwa na mshauri wa masuala ya kiuchumi katika kaunti ya Kiambu, Kasisi David Kariuki Ngari.
Kwa mujibu wa Wizara ya Biashara, Viwanda na Vyama vya Ushirika, Ekeza sasa itakubaliwa kurejelea biashara zake japo kwa masharti kuwa ni lazima dili zake zote za kifedha ziwe zikiidhinishwa na serikali.
Hii ni baada ya miaka miwili ya kuwekewa masharti ya kileseni na ambapo Ekeza haijakuwa na uwezo wa kuhudumu kama kampuni ya uwekezaji.
Mnamo Desemba 17, 2018, Kamishna wa Vyama vya Ushirika, Bi Mary Mungai aliunda kamati ya kuchunguza muundo wa kibiashara wa Ekeza kwa nia ya kuafikia maamuzi ya kurejeshewa au kunyimwa leseni.
Ni katika hali hiyo ambapo Bi Mungai amethibitisha kuwa Alhamisi ijayo kutaandaliwa mkutano wa serikali na wanahisa wa Ekeza ili kuwapa ripoti ya uchunguzi na mapendekezo.
“Mkutano huo utakuwa katika uwanja wa kitaifa wa Kasarani na ambapo waalikwa ni baadhi ya wateja wa Ekeza, wasimamizi wa Ekeza na serikali na ambapo tutatoa makubaliano ya jinsi ya kuendelea mbele kibiashara huku tukitoa hakikisho kuwa hakuna pesa za wateja wetu ambazo zitazama katika saakata hii ambayo imetuandama kwa miaka miwili sasa,” akasema Kasisi Ngari.
Upanuzi
Kwa mujibu wa Bi Mungai, shida kuu ya Ekeza ilikuwa katika upanuzi wake ambapo licha ya kuwa na leseni ya kuhudumu katika eneo la Starehe Jijini Nairobi, kampuni hiyo ilipanua harakati zake hadi katika zaidi ya kaunti 10 hapa nchini.
Pia, Ekeza ikawa na kampuni ya kando na ambayo ni ile ya ununuzi na uuuzaji mashamba ya Gakuyo Real Estate na ambapo hakuna rekodi za utendakazi zilikuwa zikiandaliwa kwa serikali kwa mujibu wa mwongozo wa vyama vya ushirika, hali ambayo ilisababisha changamoto kuu ya kupokonywa leseni kwa muda.
Kupokonywa leseni kulizindua misururu ya washirika wa uwekezaji kuanza kutoa pesa zao kwa akaunti na ambapo shida za kifedha ziliandama Ekeza kwa kasi kiasi cha kuzama.
“Hali bado inaweza ikalainishwa. Katika Ekeza, tulikuwa na hifadhi ya Sh2.5 bilioni za wateja lakini katika misukosuko iliyojiri, wanachama wengine walitoa Sh500 milioni kutoka akaunti zao na hivyo basi tukajipata bila uthabiti wa uwekezaji,” akasema Kasisi Ngari.
Huku wanachama wengine wakizidi kusukuma warejeshewe pesa zao, Ekeza imelipa Sh116 milioni lakini katika kampuni ya Gakuyo Real Estate kukiwa na mikataba ya mikopo ya Sh1.3 bilioni.
“Hali hii inakuonyesha waziwazi kuwa tuko na changamoto ndio, lakini pia tuko na uthabiti wa kimsingi. Changamoto kuu ni kuwa majina ya kampuni zetu yameharibiwa sifa mitandaoni kiasi kwamba hata kupata mwekezaji wa kushirikiana naye kumekuwa na ugumu,” akasema Kasisi Ngari.
Hata hivyo, alisema kuwa ana matumaini kuwa mambo yatalainika baada ya kuonyesha wateja wake kuwa hakuna nia yoyote ya kuzamisha akiba zao.