Habari

Mahakama yapiga breki utekelezaji sheria za kudhibiti mitandao ya kijamii

Na RICHARD MUNGUTI October 23rd, 2025 Kusoma ni dakika: 2

SERIKALI ya Rais William Ruto imepata pigo kuu baada ya Mahakama Kuu kupiga breki kutekelezwa kwa Sheria ya Kudhiti Mitandao ya Kijamii na Matumizi ya Kompyuta iliyotiwa sahihi na Rais William Ruto Oktoba 15, 2025 hadi kesi iliyowasilishwa kortini isikizwe na kuamuliwa.

Jaji Lawrence Mugambi mnamo Jumatano Oktoba 22, 2025 alitoa agizo la kusitisha kutekelezwa kwa Kifungu nambari 27(1)(b), (c) na (2) cha matumizi mabaya ya mitambo ya kompyuta na uhalifu wa kimitandao ya mwaka wa 2024.

“Kabla ya kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi iliyoshtakiwa na mwanamuziki Reuben Kigame na tume ya kitaifa ya kutetea haki za binadamu (KHRC), utekelezaji wa Sheria nambari 27(1)(b), (c), na (2) ya matumizi mabaya ya kompyuta na uhalifu wa kimitandao ya mwaka wa 2025 imesitishwa,” Jaji Mugambi aliagiza.

Agizo hilo lilitolewa kufuatia kesi iliyoshtakiwa na Bw Kigame na KHRC Oktoba 21, 2025 ikipinga kutiwa sahihi kwa sheria na Rais Ruto Oktoba 15, 2025 siku ambayo kinara wa ODM Raila Odinga aliaga dunia.

Kwa mujibu wa walalamishi hao wawili — Kigame na KHRC — sheria hiyo inakinzana na Katiba na kutweza sheria ya kulinda haki ya kibinafsi ya kila mtu (DPA).

“Mabadiliko yaliyofanyiwa sheria za kudhibiti mitandao ya kijamii na DPA inakinzana na Katiba,” walalamishi hawa walieleza mahakama.

“Kuharamishwa kwa vipengee katika sheria ya mawasiliano kunakandamiza uhuru wa kuzugumza na kujieleza,” Bw Kigame na KHRC wameeleza korti.

Pia wamesema matakwa kwamba majina ya waliofungua mitandao ya kijamii yalingane na yale yako katika kitambulisho cha kitaifa hayana mashiko kisheria.

Mahakama imeelezwa mabadiliko yaliyofanyiwa sheria hii ya mawasiliano na udhibiti wa mitandao ya kijamii yanaanika wenye mitandao hii na kupelekea kudugua sheria ya DPA.

Pia walalamishi hawa wawili wamesema mabadiliko yamevuruga uhuru wa usemi uliopewa Wakenya katika Katiba na DPA.

“Mabadiliko yaliyofanywa sio laini na yanakinzana na Kifungu nambari 24 (2) cha Katiba kinachofafanua kwa mapana na marefu haki za kila mmoja,” kesi hizo zimedai.

Sheria hii mpya ya kuharamisha mitandao ya kijamii na matumizi mabaya ya kompyuta inakinzana na Vifungu 10, 24, 33, 34, 35, 36 na 47 vya Katiba.

Bw Kigame na KHRC wanaomba mahakama kuu iifutilie mbali.