Wakili ataka IEBC ichapishe rekodi za uhalifu za wagombeaji ‘kusaidia wapiga kura’
WAKILI mmoja wa Nairobi amefika mahakamani kusaka agizo la kuilazimisha Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) kuchapisha maelezo kuhusu rekodi za uhalifu za wagombeaji kabla ya wao kushiriki katika chaguzi zijazo.
Bw Harry Stephen Arunda anasema maelezo kuhusu mashtaka yao, hukumu au ikiwa waliachiliwa huru au iwapo mgombeaji anayo kesi mahakamani yatawasaidia wapiga kura kufanya uamuzi.
Anaongeza kuwa wapiga kura wanafaa kupata maelezo kuhusu mapato, mali na madeni na historia ya mgombeaji kuhusu ulipaji ushuru ili wafanye uamuzi bora debeni.
Wakili Arunda anasema kuwa maelezo kama hayo muhimu kuhusu wagombeaji yanapasa kuchapishwa na IEBC kabla ya kufanyika kwa uchaguzi.
“Maelezo hayo pia yanafaa kuhusisha elimu ya mgombeaji na uwezo wake wa kutekeleza majukumu ya afisi anayowania,” akaeleza.
Bw Arunda alisema kuwa endapo IEBC itatoa maelezo kama hayo, basi itazuia hali ya sasa ambapo watu wanaibuka na kutoa kauli za uwongo kuhusu uwezo wao wa kutekeleza majukumu ya nyadhifa mbalimbali za uongozi “kinyume na misingi ya kidemokrasia na utawala bora nchini.”
Jaji Chacha Mwita aliamuru Bw Arunda kuwasilisha stakabadhi za kesi hiyo kwa wahusika wote ikiwemo IEBC, Mwanasheria Mkuu Dorcas Oduor, Bunge na Afisi ya Msajili wa Vyama vya Kisiasa.
Kesi hiyo itatajwa mnamo Novemba 10, ambapo maagizo zaidi yatatolewa.Wakili Arunda pia anaitaka mahakama kuu kuamuru Msajili wa Vyama vya Kisiasa kuchapisha mikataba ya miungano iliyowekwa katika afisi yake, kabla ya chaguzi kufanyika.
“Mlalamishi anahoji ikiwa kushiriki kwa raia katika chaguzi ni aina ya ushirikishaji wa umma na hivyo kwafaa kuendeshwa kwa uzingativu wa mahitaji ya vipengele vya 10, 32 (1), 33, na 35 vya katiba,” akasema Bw Arunda.
Wakili huyo alisema ni muhimu kwa raia kujua mapema maelezo muhimu kuhusu wawaniaji wanaoshiriki katika chaguzi.
Kulingana na wakili Arunda hata baada ya wagombeaji wa viti mbalimbali kuidhinishwa na IEBC, raia huwa hawafahamu mengi muhimu kuwahusu ili waweze kufanya maamuzi bora wanapopiga kura.