UDA kumwadhibu gavana Kahiga
CHAMA cha United Democratic Alliance (UDA) sasa kitamwadhibu Gavana wa Kaunti ya Nyeri, Mutahi Kahiga kwa matamshi yake ya ‘kusherehekea’ kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu wa zamani hayati Raila Odinga.
Akizungumza Alhamisi, Oktoba, 23, 2025, mwenyekiti wa chama hicho Cecily Mbarire alisema kuwa chama hicho hakitajihusiha na matamshi yake.
“Kama chama cha UDA, tunajitenga kabisa na matamshi ya Bw Kahiga,” alisema Bi Mbarire.
Hii ni baada ya matamshi ya kiongozi huyo kukashifiwa vikali na viongozi mbalimbali nchini.
Wiki hii, kiongozi huyo alirekodiwa akitoa matamshi yanayoashiria kuwa anasherehekea kifo cha Bw Odinga.
Viongozi sasa wanataka Bw Kahiga afunguliwe mashtaka.
Wenzake katika Baraza la Magavana (CoG), na viongozi wa ODM Gavana Simba Arati (Kisii) na Bi Gladys Wanga (Homa Bay) wamesikitishwa na maneno yake wakati nchi bado inaomboleza kifo cha Raila.
Bi Wanga alihusisha maneno ya Gavana huyo na aliyekuwa Naibu rais Rigathi Gachagua, akimlaumu kwa kueneza chuki na kutokuwa na heshima kwa Odinga, alipokuwa hai na sasa akiwa amekufa.
“Tunaka akamatwe mara moja na kufunguliwa mashtaka kwa maneno yake kuhusu kifo cha Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga,” alisema Gavana Arati, akiongeza kuwa “maneno kama hayo yanalenga kugawanya Kenya.”