Makala

Mashirika yataka sanamu ya kumuenzi Raila ijengwe katika Bunge la Kitaifa

Na JOSEPH WANGUI, BENSON MATHEKA October 25th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

MUUNGANO wa mashirika ya kijamii umewasilisha ombi katika Bunge la Kitaifa kutaka sanamu ya hayati Waziri Mkuu wa zamani Raila Odinga ijengwe katika eneo la majengo ya Bunge, wakisema mchango wake mkubwa katika demokrasia, mageuzi ya kikatiba na utetezi wa haki za binadamu unastahili heshima ya kudumu.

Wakiongozwa na Peter Agoro, mwenyekiti wa Consortium of Civil Societies in Kenya, viongozi wa mashirika ya kijamii wanadai kuwa urithi wa Odinga wa zaidi ya miongo minne unastahili kutambuliwa sawa na mashujaa wengine wa kitaifa kama Field Marshal Dedan Kimathi na Tom Mboya.

Ombi hilo limekitwa katika mchango wa Odinga katika mageuzi ya kisiasa nchini, utetezi wa haki za wanyonge, usawa wa kijinsia, na kulinda haki za binadamu pamoja na utawala wa sheria.

Wanamtaja Odinga kama “Baba wa Demokrasia,” “Mtetezi wa Wanawake,” “Mlinzi wa Haki za Binadamu,” na “Mwanamageuzi wa Ugatuzi” na  sanamu hiyo itakuwa ishara ya kudumu ya mchango wake.

“Kama mtetezi wa usawa wa kijinsia, Bw Odinga amekuwa akihimiza fursa sawa katika nyanja za kisiasa, kiuchumi na kijamii, akitekeleza roho ya Ibara ya 27(3) ya Katiba kuhusu usawa na kanuni ya theluthi mbili chini ya Ibara ya 81(b),” linasema ombi hilo.

Pia wanasema kuwa uongozi wake wa bara la Afrika na ushawishi wa kimataifa umeinua hadhi ya Kenya kimataifa, sambamba na Ibara za 2(5) na (6) za Katiba zinazohusu mikataba ya kimataifa.

Wametaja mchango wake katika kuandikwa kwa Katiba ya 2010, muafaka wake na rais Mwai Kibaki wakati wa mgogoro wa kisiasa wa mwaka 2007/2008, na mapambano yake ya muda mrefu ya kuanzisha siasa za vyama vingi na ugatuzi.

“Licha ya mchango wake mkubwa, Kenya haina alama ya kitaifa inayomheshimu,” lilisema ombi hilo.

Kwa mujibu wa Bw Agoro, kujenga sanamu ya Odinga katika majengo ya Bunge “kutakuwa dira ya maadili kwa wabunge,” kuwakumbusha kila siku kuhusu misingi ya kidemokrasia aliyopigania.

“Sanamu hiyo itawahamasisha wabunge kutetea misingi ya Katiba na kuepuka kupitisha sheria kandamizi zinazoweza kudhoofisha demokrasia, haki za binadamu, vyama vingi na ugatuzi alivyosimamia,” alisema Bw Agoro.

Ombi hilo linanukuu Ibara ya 11 ya Katiba inayohimiza utamaduni na sanaa kama sehemu ya urithi wa kitaifa, na Ibara ya 119 inayotoa haki kwa raia kuwasilisha ombi bungeni.

Pia linaeleza mifano ya kimataifa kama Lincoln Memorial nchini Amerika na sanamu ya Winston Churchill nchini Uingereza, likisema alama kama hizo huimarisha umoja wa kitaifa na kuelimisha vizazi vijavyo kuhusu historia.

“Sanamu kama hizi huchochea fahari ya kitaifa na kuongeza uelewa wa kihistoria, zikitekeleza Ibara ya 11(2) ya Katiba kuhusu kukuza urithi wa kitamaduni kupitia sanaa,” ombi hilo linaongeza.

Mashirika hayo yanasema yamepata uungwaji mkono mkubwa kutoka kwa asasi za kiraia, vijana na wanasiasa wa pande zote za kisiasa, wakisisitiza kuwa mchango wa Odinga unavuka mipaka ya kisiasa.

Wanasema sanamu hiyo itakuwa kiunganishi cha vizazi, ikihamasisha viongozi wa baadaye na kuimarisha uzalendo na umoja wa kitaifa kulingana na Ibara ya 10 ya Katiba.

Bunge limepokea rasmi ombi hilo, na sasa inatarajiwa kushughulikiwa kwa mujibu wa taratibu za kikatiba.

Iwapo litakubaliwa, sanamu ya Raila Odinga itakuwa miongoni mwa nyingine za kitaifa zinazotambua mashujaa wa ukombozi na vinara wa kisiasa nchini.

“Wakati umefika wa kuhifadhi urithi wa Raila Odinga,” alisema Bw Agoro, akiwa na mwenzake John Wangai. “Hii si heshima tu kwa mtu mmoja bali ni njia ya kulinda safari ya kidemokrasia ya Kenya na kuizuia kurudi nyuma kisheria na kisiasa.”