Watafiti wagundua kinachopunguza uwezo wa wanawake kupata mimba
UWEZO wa mwanamke kupata mimba hupungua kwa kasi kuanzia katikati ya umri wa miaka 30, jambo ambalo limekuwa likiwasumbua wanasayansi kwa muda mrefu.
Kwa miaka mingi, watafiti waliamini kuwa chanzo kikuu cha kupungua kwa uwezo huu ni ubora wa mayai. Hii ni kwa sababu wanawake huzaliwa na idadi ya mayai watakayokuwa nayo maisha yote, na kadri wanavyokaribia kukoma hedhi, idadi na ubora wa mayai hayo hupungua.
Hata hivyo, utafiti mpya umebainisha kuwa si ubora wa mayai pekee unaochangia kushuka kwa uwezo wa uzazi, bali pia mabadiliko katika seli na tishu za ovari. Matokeo haya yanaweza kubadilisha uelewa wa kisayansi kuhusu mfumo wa uzazi na njia za kuhifadhi uwezo wa kuzaa.
Utafiti kuhusu uzazi wa wanawake ni changamoto kubwa, kwani kwa muda mrefu umekuwa ukifadhiliwa kwa kiwango cha chini, na pia ni vigumu kuchunguza kwa sababu ovari ni kiungo kigumu kufikiwa. Kwa hivyo, wanasayansi mara nyingi hutumia wanyama kama panya, ambao baiyolojia yao inafanana na binadamu.
Katika utafiti huu, watafiti walilinganisha tishu za ovari za panya wachanga na wazee na zile za wanawake wenye umri wa miaka 20, 30 na 50. Kwa kutumia teknolojia ya picha za 3D na uchambuzi wa vinasaba, waliunda ramani za kina za aina za seli na kazi zake katika kipindi cha maisha ya mwanamke.
Waligundua kwamba ingawa kuna tofauti kati ya ovari za binadamu na panya, kuna uwiano mkubwa katika jinsi mayai na seli zinazozunguka yai zinavyofanya kazi. Seli hizi huzalisha homoni ya oestrogen kwa wanawake, na panya wana seli zenye kazi sawa.
Hata hivyo, ambazo kwa binadamu huzalisha testosterone zilionyesha kufanya kazi kwa njia tofauti kwa panya.
Utafiti huo pia ulionyesha kuwepo kwa seli maalum za neva zinazoitwa glial cells ndani ya ovari za panya na binadamu, ambazo huanza kukua mapema wakati wa ujauzito. Seli hizi huchochea ovari kutengeneza mayai. Watafiti walipozitengeneza upya kwa njia ya kimaumbile katika panya, waliona matokeo yanayofanana na ugonjwa wa polycystic ovarian syndrome (PCOS) ambapo mayai mengi ya awali hukua lakini hushindwa kukomaa ipasavyo.
Kwa kulinganisha ovari za vijana na wazee, watafiti waligundua kuwa tishu za ovari za binadamu huwa ngumu zaidi kadri miaka inavyoongezeka, kutokana na mabadiliko ya nyuzi za tishu na michakato ya upasuaji wa asili unaotokea baada ya kila mzunguko wa kutoa mayai. Hii ndiyo huenda inasababisha wanawake kupoteza uwezo wa kuzaa mapema kuliko wanyama wengine.
Matokeo haya yanaashiria kwamba kushuka kwa uwezo wa kuzaa hakusababishwi tu na ubora wa mayai, bali na mfumo mzima wa tishu na seli zinazounda ovari. Watafiti wanasema ufahamu huu unaweza kusaidia kubuni tiba mpya za matatizo ya uzazi na utasa.
Kwa mara ya kwanza, wanasayansi wana matumaini kwamba kutumia mifumo ya wanyama maabara kutawezesha utafiti mpana zaidi wa afya ya wanawake, eneo ambalo kwa miaka mingi limepuuzwa na kufadhiliwa kwa kiwango cha chini.
“Uelewa huu mpya utasaidia kuboresha matibabu, kuzuia matatizo ya uzazi, na kuhifadhi uwezo wa kuzaa kwa wanawake,” utafiti huo unasema