Wakili adai alipoteza wateja alipotishiwa na Sonko
Wakili mmoja amedai katika Mahakama Kuu ya Nairobi kwamba alijiondoa kama msimamizi na mdhamini wa mali yenye thamani ya Sh 50 bilioni ya marehemu James Simon Bellhouse, baada ya kutishwa na aliyekuwa Gavana wa Nairobi, Mike Sonko.
Wakili Lucy Nyamoita Momanyi aliiambia mahakama kwamba Sonko alimkabili katika Mahakama Kuu ya Mombasa akimlaumu kwa “matumizi mabaya ya mamlaka” katika usimamizi wa urithi huo mkubwa, hatua iliyomfanya kujiuzulu kwa hofu ya usalama wake.
Kulingana na stakabadhi za mahakama, wosia wa marehemu Bellhouse ulioandikwa Januari 10, 2007, ukimtaja Bi Momanyi na mjane wa marehemu, Joy Nadzua Bellhouse, kama wasimamizi wa mali hiyo. Marehemu pia aliagiza azikwe katika shamba lake la Shimba Hills, Kaunti ya Kwale, kwa taratibu za Kikristo.
Bellhouse alifariki mwaka 2009 na mali zikiwemo ekari 80 za ardhi ya ufuo wa bahari Diani, ya thamani ya Sh48 bilioni, pamoja na hisa katika kampuni kadhaa nchini.
Bi Momanyi anaomba mahakama imuamuru Sonko kuacha kumzungumzia yeye au kampuni yake ya uwakili ya L.N. Momanyi & Company Advocates, kuhusiana na usimamizi wa urithi huo. Pia anadai fidia kwa kuchafuliwa jina na na gharama ya kesi.
Akitoa ushahidi wake Oktoba 23, 2025, wakili huyo alidai kuwa matamshi ya Sonko yaliyochapishwa kwenye vyombo vya habari yalimharibia sifa na kumfanya apoteze wateja.
“Nilipoteza wateja kutokana na maneno aliyosema dhidi yangu, na hivyo nikapata hasara kubwa,” aliambia jaji.
Hata hivyo, Sonko kupitia kwa wakili wake alipinga madai hayo, akisema hakumtukana wala kumharibia jina Bi Momanyi.
Katika kiapo chake cha utetezi, Sonko anadai kwamba mjane wa Bellhouse alimuomba amsaidie baada ya kugundua mali ambayo haikuorodheshwa kwenye wosia huo, na kwamba wosia uliodaiwa kuandaliwa na Bi Momanyi “haukutekelezwa ipasavyo” kisheria.

“Nilipotaka ufafanuzi kutoka kwake, alinikwepa na hata akamwonya mjane kutowasiliana nami ikiwa angetaka kurithi mali,” Sonko anasema katika kiapo chake.
Sonko anadai kuwa baadhi ya mali ya marehemu haikutajwa kwenye wosia huo na kwamba tabia ya Bi Momanyi ilisababisha migogoro kati yake na mjane wa marehemu. Pia anasema alishauri mjane kuripoti kwa polisi madai kwamba wakili huyo alimtolea vitisho, jambo lililofanywa chini ya OB No. 47/3/047 katika Kituo cha Polisi cha Diani.
Wakati wa kuhojiwa na mawakili wa Sonko, Bi Momanyi alikiri kuwa mbali na makala moja ya Juni 2010, hakuna chapisho jingine lililotolewa na Sonko dhidi yake.
Sonko pia alimwambia jaji kwamba wakili huyo ndiye kwanza aliyetoa taarifa za kumchafulia jina, akidai kwamba yeye “ni mhalifu aliyehusika katika kumtapeli Sh16 milioni.”
“Ni kweli mimi nilijibu tu madai hayo kwa kusema ana nia ya kumpora mjane mali ya marehemu Bellhouse,” Sonko alisema mahakamani.
Sonko anaomba mahakama kutupilia mbali kesi hiyo akidai haina mashiko, akisema mlalamishi amechochewa kisiasa na hana ushahidi wa kuonyesha alipoteza wateja kutokana na matamshi yake.
“Wewe hujaonyesha ushahidi wowote kwamba ulipoteza wateja. Hivyo madai hayo ni ya kubuni,” wakili wa Sonko alimwambia Bi Momanyi.
Bi Momanyi alisisitiza kwamba alipoteza wateja wa mashirika na atawasilisha ushahidi kuthibitisha hilo..
Kesi hiyo itaendelea kusikizwa Oktoba 27, 2025.