Makala

Fahamu malengo ya Sheria ya makosa ya kingono na haki kwa waathiriwa

Na BENSON MATHEKA October 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Safari ya kuanzishwa kwa Sheria ya Makosa ya Kingono nchini Kenya ilikuwa mchakato mrefu, mgumu na uliojaa changamoto nyingi, uliochukua miongo kadhaa kabla ya kufanikisha mabadiliko makubwa ya kisheria.

Ulianza mwanzoni mwa miaka ya 1990, wakati matukio makubwa ya ukatili wa kingono yalipotokea, ikiwemo tukio la mwaka 1991 katika Shule ya Mseto ya St. Kizito, Meru, ambapo wasichana wengi walifanyiwa unyama wa kingono na baadhi yao walikufa. Tukio hili lilionyesha jinsi sheria zilizokuwepo zilivyokuwa hafifu na hazikutoa msaada wa kutosha kwa wahanga.

Hali hii ilizua hisia kali za hasira na wito wa haraka wa mabadiliko ya kisheria ili kulinda haki za wanawake na watoto dhidi ya unyanyasaji wa kingono.

Wanaharakati wa haki za binadamu walijitokeza kuanzisha kampeni za kupigania mabadiliko ya sheria za ukatili wa kingono. Waligundua kuwa sheria zilizokuwepo hazikuwa na ufafanuzi wa kutosha wa makosa ya kingono, na adhabu kwa wahalifu ilikuwa hafifu sana, mara nyingi ikiwaruhusu kuepuka adhabu.

Hali hii ilisababisha mashirika mbali mbali kuanzisha mazungumzo, ikiwemo FIDA-Kenya na Mtandao wa Haki za Watoto (JJN), ambayo yalifanya kazi kwa karibu na Idara ya Sheria na Bunge kuanzisha marekebisho.

Mbali na hayo, yalifanya uhamasishaji mkubwa kwa jamii ili kubadilisha mtazamo hasi kuhusu unyanyasaji wa kingono na kuondoa aibu inayowapata wahanga.

Marekebisho ya Sheria ya Jinai ya 2001 yaliibuka kama hatua ya kwanza, lakini yalihitaji kuimarishwa zaidi ili kushughulikia makosa ya kingono kwa kina na kuwapa wahanga haki zaidi.

Baada ya changamoto nyingi, Mbunge Njoki Ndung’u aliibua hoja ya kuleta mswada wa Sheria ya Makosa ya Kingono kama Mswada wa Mwanachama Binafsi bungeni mwaka 2004, huku akisaidiwa na kampeni za umma na mashirika ya kiraia. Njoki Ndung’u alikumbana na upinzani mkubwa kutoka kwa baadhi ya wabunge waliokuwa na mtazamo wa kijinsia wa jadi, lakini alishikilia msimamo wake kwa ajili ya haki na usawa wa kijinsia.

Kampeni za umma zilihusisha mijadala ya redio, televisheni, makongamano, na kuandika makala katika vyombo vya habari ili kuhamasisha umuhimu wa sheria hiyo na athari za ukatili wa kingono kwa jamii.

Hii ilisababisha shinikizo kubwa kwa wabunge na serikali ili mswada upitishwe. Pamoja na changamoto hizo, walifanikiwa kuhamasisha umma na kupata msaada wa vikundi mbalimbali vya wanawake, vyombo vya habari, na watu maarufu.

Hatimaye, kutokana na jitihada hizo, Sheria ya Makosa ya Kingono ilipitishwa na kuleta mabadiliko makubwa hasa haki kwa wahanga wa ukatili wa kingono, kuimarisha vifungu vya adhabu kwa wahalifu na kutoa ufafanuzi mpana wa makosa haya nchini Kenya.

Sheria hii imekuwa msingi muhimu katika mapambano dhidi ya ukatili wa kingono nchini na kuimarisha haki za wanawake na watoto. Aidha, imechangia kuongeza uelewa wa jamii kuhusu haki za binadamu na umuhimu wa kuheshimu utu wa kila mtu, ikizingatia kuwa ukatili wa kingono ni kinyume cha haki za binadamu na lazima ukome kabisa.