Makala

Fahamu kinachochea uraibu wa mitandao ya kijamii

Na BENSON MATHEKA October 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Huenda hujui kuna njia zilizothibitishwa kisayansi za kupambana na athari mbaya za afya ya akili na hisia katika  ulimwengu wenye kasi ya dijitali.

Wataalamu wa malezi dijitali wanasema kuna tafiti za kuwasaidia vijana kuishi maisha yenye furaha, afya, na usawa zaidi katika ulimwengu huu wa tekinolojia.

“Wazazi hawataki watoto wao wahisi kutengwa kijamii. Tunajua kuwa mitandao ya kijamii ina faida, kutokana na matumizi yetu wenye afya ya mitandao ya kijamii kuwasiliana na marafiki. Wazazi wanaweza kuhisi wasiwasi wa watoto wao wanapowakausha kutumia simu zao za mkononi, na takwimu zinaonyesha vijana wanahisi kutengwa sana wanapokosa simu zao kabisa,” asema mtafiti wa malezi dijitali Amira Rezek.

Wazazi, asema, wanafaa kuwasaidia watoto wao wapate faida za mawasiliano mtandaoni kupitia matumizi salama na yenye afya ya mitandao ya kijamii, lakini pia wanafaa kuwalinda dhidi ya athari mbaya zinazoweza kutokea kutokana na matumizi mengi ya vyombo vya kidijitali.

 “Athari hizo mbaya ni pamoja na kupungua kwa muda wa umakini, uraibu mtandaoni (pamoja na kamari kwa vijana), kujilinganisha kihisia, unyanyasaji mtandaoni, au kuchukua nafasi ya shughuli zenye afya na faida kama mazoezi ya mwili, kuwasiliana ana kwa ana na watu, au kusoma vitabu na matumizi ya vyombo vya kidijitali visivyo na faida,” aeleza Amira.

Anasema baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa afya duni ya akili ndiyo inayochochea matumizi ya mitandao ya kijamii kuongezeka na hivyo basi wazazi wana jukumu la kuthibiti wanao kuitumia.

“Badala ya kuwa na msongo wa mawazo na wasiwasi kuhusu jinsi matumizi ya vyombo vya kidijitali na mitandao ya kijamii yanavyoathiri watoto wetu, tunaweza kuchukua hatua madhubuti kujifunza hisia za watoto wetu kuhusu maisha na shule. Vijana mara nyingi hukataa kusema wanavyohisi kwa wazazi kwa hofu ya kuwakatisha tamaa. Uhusiano mzuri na wazazi hupunguza hatari za afya ya akili zinazohusiana na mitandao ya kijamii. Hii ndiyo sababu kubwa ya kukuza uhusiano mzuri kati yako na watoto wako,” asema.

Wataalamu wanasema kwamba japo walimu wanahakikisha wanafunzi wanapata huduma kamili za kisaikolojia wanazohitaji kufanikiwa, watoto wanahitaji zaidi ya huduma za shule.

Kwa mfano, hakuna wasaikolojia wa shule wa kutosha kusaidia watoto wote katika shule kudumisha afya bora ya kisaikolojia.

Watoto wanaweza kufaidika na mabadiliko chanya yanayoathiri afya yao ya akili kwa ujumla. Hata kama afya ya akili ya mtoto wako inaonekana kuwa nzuri, unaweza kuiboresha kupitia mazungumzo  na michezo  ili kupambana na athari mbaya zinazoweza kusababishwa na vyombo vya kidijitali.