Ushauri nasaha unasafisha ndoa
Ndoa ni safari yenye mseto wa changamoto na vicheko, na wakati mwingine majonzi. Wataalamu wa mahusiano wanasema kuwa mapenzi pekee hayatoshi kudumisha ndoa; kunahitajika mawasiliano bora, uvumilivu, na mara nyingi msaada wa kitaalamu kupitia ushauri nasaha.
Katika jamii nyingi, wanandoa wengi hushindwa kutafuta msaada wa ushauri hadi mambo yanapokuwa mabaya. Wengine huona aibu au hofu kwamba watu watadhani ndoa yao inavunjika wakiomba ushauri wa wataalamu. Lakini wataalamu wanasema kuwa huo ni mtazamo potofu unaowazuia wengi kurekebisha na kufurahia ndoa.
“Ushauri nasaha haukusudiwi kwa wanandoa waliokaribia kuachana pekee,” anasema Bi Margaret Njoroge, mshauri wa familia jijini Nairobi. “Ni nafasi ya kujifunza jinsi ya kuelewana, kusamehe, na kuboresha urafiki ndani ya ndoa.”
Anasisitiza kuwa changamoto nyingi katika ndoa hutokana na mawasiliano hafifu. Wanandoa wengi hushindwa kuelezea hisia zao kwa uwazi au hufasiri vibaya maneno ya wenzao. Kupitia ushauri nasaha, wanandoa hufundishwa jinsi ya kuzungumza kwa heshima na kusikilizana bila hukumu
“Ndoa nyingi zinaharibika si kwa sababu ya ukosefu wa upendo, bali kwa sababu ya ukosefu wa mazungumzo,” anasema Mchungaji Daniel Obuya, mshauri wa mahusiano. “Ushauri unafungua milango ya mazungumzo, unavunja ukuta wa ukimya na hofu.”
Kila mtu huja katika ndoa akiwa na historia, malezi na matarajio tofauti. Wengine wanaamini mapenzi ni maneno matamu; wengine huona ni vitendo au uaminifu wa kifedha. Wakati matarajio haya yanapogongana, migogoro huzuka.
Kupitia ushauri, wanandoa hufundishwa jinsi ya kuelewa na kuheshimu tofauti hizo bila kuumizana. Ushauri hutoa nafasi ya kuuliza maswali magumu kama vile: “Kwa nini ninahisi kutoeleweka?” au “Je, ninawezaje kumpenda zaidi licha ya makosa yake?”
Wataalamu wanasema, ushauri bora zaidi si ule unaokuja baada ya matatizo, bali ule unaosakwa kabla mambo hayajaharibika.
“Wanandoa wanapaswa kufika kwa mshauri hata wakati mambo yanaenda vizuri,” anasema Bi Lucy Wanjiku, mshauri wa mahusiano na mwandishi wa vitabu vya ndoa. “Kama vile unavyokagua afya ya mwili mara kwa mara, ndoa pia inahitaji ukaguzi wa kihisia.”
Kwa kufanya hivyo, wanandoa hujifunza mbinu za kushughulikia tofauti ndogo kabla hazijageuka milima ya migogoro.
Wengi hufikiri ushauri ni kutafuta nani ana makosa, lakini ukweli ni kwamba ni nafasi ya kujitafakari. Mshauri husaidia kila upande kuona mchango wake katika matatizo ya ndoa na jinsi ya kubadilika.
“Watu wengi hushangaa wanapogundua kwamba matatizo yao yanaweza kudhibitiwa kirahisi,” asema Mzee Joseph Mwangi, mshauri wa ndoa mwenye tajriba ya zaidi ya miaka 20. “Ushauri hufungua macho, unaondoa lawama na kuleta uelewa.”
Pamoja na faida hizi, wapo wanaokataa ushauri kwa sababu ya kiburi. Wengine huona ni udhaifu au kuonekana kama wameshindwa. Lakini wataalamu wanatahadharisha kuwa kiburi ndicho kinachoua ndoa nyingi.
“Kukataa msaada kwa sababu ya kiburi ni sawa na kukataa kwenda hospitalini wakati unaumwa,” asema Bi Njoroge.
Kuna wakati mwenzi mmoja anakataa kabisa wazo la kwenda kwa ushauri. Katika hali kama hiyo, wataalamu wanashauri kwamba mmoja anaweza kwenda peke yake. Kupitia hapo, atapata ujuzi wa kushughulikia hali iliyopo na huenda akawa chanzo cha mabadiliko.
“Suluhisho la ndoa halipaswi kutokea kwa wakati mmoja kutoka pande zote mbili,” anasisitiza Mchungaji Obuya. “Wakati mwingine hatua ya mmoja tu inaweza kuokoa uhusiano.”
Anasisitiza kuwa ushauri nasaha si ishara ya udhaifu, bali ni dalili ya hekima. Ni uamuzi wa watu wawili wanaotaka kujifunza, kukua na kudumu katika upendo. Ndoa iliyo imara si ile isiyo na matatizo, bali ile wahusika wanaweza kushughulikia changamoto kwa hekima.