Makala

Uhuru asuka mikakati ya 2027 chini ya maji

Na MWANGI MUIRURI October 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

RAIS mstaafu Uhuru Muigai Kenyatta atagonga miaka 64 leo akiwa na mzigo wa urithi wa kisiasa ulioyumba na azma mpya ya kuibuka tena katika ulingo huo kuelekea kura ya 2027.

Safari yake ya kisiasa ya zaidi ya miaka 28 imejumuisha nyadhifa za ubunge, uwaziri, naibu waziri mkuu na hatimaye urais.Kisha kustaafu mwaka 2022 baada ya mgombeaji aliyempendelea, hayati Raila Odinga, kushindwa na aliyekuwa naibu wake, William Ruto.

Baada ya kushirikiana na Dkt Ruto katika uchaguzi mkuu wa 2013 na 2017, Bw Kenyatta aligeuka na kumuunga mkono Bw Odinga mwaka 2022. Hata hivyo, kura za Mlima Kenya zilimponyoka pakubwa huku Bw Ruto akipata asilimia 88 katika ngome hiyo ya Bw Kenyatta.

Licha ya hayo Bw Kenyatta bado anaonekana kama mshawishi wa kisiasa anayepanga mikakati yake chini kwa chini. Majuzi Rais Ruto alisema hadharani kwamba, “ninafanya kazi naye (Kenyatta) kuunganisha taifa.”

Bw Kenyatta, ambaye bado anaongoza chama cha Jubilee, alithibitisha kuwa kingali sehemu ya muungano wa Azimio la Umoja, uliokuwa ukiongozwa na Bw Odinga kabla ya Waziri Mkuu huyo wa zamani kupenya serikalini kupitia ODM – chama kilicho na wabunge wengi zaidi.

Rais Mstaafu na Kiongozi wa Chama cha Jubilee, Uhuru Kenyatta (kushoto) akiwa na Waziri wa zamani wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i wakati wa Mkutano Maalum wa Wajumbe wa Kitaifa wa Chama cha Jubilee uliofanyika katika Uwanja wa Mbio wa Ngong, Nairobi, Septemba 26 2025.
Picha| Bonface Bogita

Mchanganuzi wa masuala ya siasa Profesa Peter Kagwanja anaeleza kuwa, “baada ya Ruto kumshinda bosi wake kwa shida mwaka 2022 aliamua kuwaendea wapinzani wao hao – Kenyatta na Odinga – na ndani ya miaka miwili wakaafikiana kisiasa, jambo linalotikisa ulingo wa siasa hadi sasa.

”Profesa Kagwanja anahusisha makubaliano hayo na hatua ya Ruto kumuondoa Rigathi Gachagua katika wadhifa wa Naibu Rais mwaka 2024, akisema ilikuwa sehemu ya mpangilio mpya wa nguvu za kisiasa.

Mbunge wa Naivasha, Bi Jayne Kihara, anadai kuwa kambi ya Gachagua “ilisulubishwa katika msalaba wa usaliti wa kisiasa.”“Kufurushwa kwake kulifanyika ili waliokuwa wameangushwa warudi madarakani na kunyakua upya ushawishi wa Mlima Kenya,” alisema.

Katibu Mkuu wa Jubilee, Jeremiah Kioni, anasema kwamba Kenyatta “bado ndiye kiongozi halisi wa Mlima Kenya” na mtu “anayefaa kutuongoza kuelekea 2027 kulinda maslahi ya jamii yetu.”

“Watu wasielewe vibaya; Uhuru ana dira ya 2027 ya kushiriki katika ukombozi wa kizazi kipya kinachopigana kupambana na magonjwa, njaa na ujinga,” aliongeza Kioni.

Kauli yake inaakisi onyo la Francis Atwoli, Katibu Mkuu wa COTU, aliyesema mwaka 2022 kuwa, “Uhuru ni mchanga sana kustaafu siasa.”Tangu wakati huo, jina la Kenyatta halijawahi kutoweka katika mijadala ya kitaifa.

Serikali ya Ruto ilimlaumu kwa kufadhili maandamano ya baada ya uchaguzi mwaka 2023, na uvamizi wa shamba la Northlands ukachochea vita vya maneno kuhusu ni nani aliyepanga tukio hilo.

Bw Kenyatta pia alionekana kukera serikali kwa kuunga mkono maandamano yalioongozwa na kizazi cha Gen Z mwaka 2024. Serikali ilimshutumu kwa “kuwachochea vijana”.

Kwa sasa, Jubilee imemteua aliyekuwa Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i, kuwa mgombea wake wa urais 2027 huku Kenyatta akisema, “tutakutana uwanjani hivi karibuni kujadiliana kuhusu mustakabali wa taifa letu.”

Hatua hiyo imefufua uhasama wake na Rigathi Gachagua, ambaye sasa anaongoza chama kipya cha Democracy for Citizens Party (DCP). Gachagua ameunda muungano wa “vyama vya Mlima Kenya” akishirikiana na Martha Karua (People’s Liberation Party), Justin Muturi (Democratic Party) na Mithika Linturi, kuunganisha kura za eneo hilo.

“Uhuru anawakilisha jana na amestaafu, mimi ndiye wa sasa na kesho ya Mlima,” Gachagua alinukuliwa akisema ishara kuwa vita vya uongozi wa Mlima Kenya bado vinaendelea.Kenyatta amebaki kimya hadharani, lakini wachambuzi wanasema ukimya wake ni wa kimkakati.

Katika umri wa miaka 64, bado anaonekana kuwa nguvu zilizojificha, mpanga mikakati ya kisiasa na mfalme anayeongoza kwa kimya.