Habari za Kitaifa

Baraza Kuu ya ODM kukutana kwa mara ya kwanza bila Raila

Na JUSTUS OCHIENG', KASSIM ADINASI October 26th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

Chama cha Orange Democratic Movement (ODM) kinajiandaa kwa mkutano muhimu wa Baraza Kuu Simamizi Jumatatu, Oktoba 27, ili kupitia upya ratiba ya sherehe za maadhimisho ya miaka 20 tangu kuanzishwa kwake, na pia kujadili mwelekeo wa chama wakati huu wa mvutano wa urithi kufuatia kifo cha Raila Odinga.

Ratiba ya hafla hizo ilivurugika baada ya kifo cha Bw Odinga mnamo Oktoba 15, siku ambayo hafla ilikuwa imepangwa kufanyika Kaunti ya Kajiado, huku hafla ya Oktoba 26 ikipangwa kufanyika Turkana.

Mwenyekiti wa maadhimisho ya ODM@20, Mbunge wa Suna Mashariki Junet Mohamed, na Naibu Kiongozi wa ODM, Godfrey Osotsi, wamethibitisha kuwa mkutano huo wa Jumatatu utakuwa wa kwanza tangu kifo cha Bw Odinga.

Mkutano huo unafuatia ule wa Kamati Kuu ya Kitaifa (NEC) uliofanyika wiki iliyopita, ambapo Seneta wa Siaya, Dkt Oburu Oginga, aliidhinishwa kuwa Kaimu Kiongozi wa ODM.

Jana, Bw Junet aliambia Taifa Jumapili kuwa maadhimisho hayo yataendelea kama yalivyopangwa, yakihitimishwa kwa tamasha la siku tatu jijini Mombasa. “Chama kitatoa ratiba mpya ya maadhimisho ya ODM@20 baada ya kikao cha Jumatatu. Sherehe zitaendelea,” alisema Bw Junet.

Kwa upande wake, Bw Osotsi alisema ajenda ya mkutano huo haitakuwa nzito kwani wanachama bado wako kwenye maombolezo. “Tutazungumzia zaidi umoja wa chama na uchaguzi mdogo unaokuja. Maamuzi makubwa yatafanyika baada ya kipindi cha maombolezo cha siku 30 kumalizika,” alieleza.

Alipuuzilia mbali madai ya mivutano ya ndani kuhusu msimamo mkali wa Katibu Mkuu Edwin Sifuna dhidi ya muundo wa serikali jumuishi, na fununu kwamba huenda akavuliwa wadhifa wake. “Maamuzi kama hayo makubwa hayapaswi kufanywa sasa. Watu bado wanaomboleza. Lengo kuu sasa ni kuunganisha chama na kuendelea na maono ya Baba,” alisema.

Akimtetea Bw Sifuna, Bw. Osotsi alisema matamshi yake yanaendana na msimamo wa chama. “Sifuna hajakiuka chochote. Tulikubaliana kuwa tupo ndani ya serikali hii ya pamoja hadi 2027, na hilo ndilo Raila alisema kila mara,” aliongeza.

Aidha, alihimiza chama kutilia mkazo ajenda ya msingi ya ushirikiano kati ya ODM na UDA yenye nguzo 10, akisema ndiyo “gundi inayoshikilia serikali hii jumuishi.” Alitaka pia kusisitizwa kwa suala la vijana waliokamatwa au kujeruhiwa wakati wa maandamano ya awali, akisema kuwa kuachiliwa kwao ni jambo la kipaumbele katika mazungumzo yajayo.