Kenya yapewa kibali kushtaki jeshi la Uingereza
UINGEREZA imekubali kuwa Kenya inaweza kuwafungulia mashtaka wanajeshi wake waliotuhumiwa kwa makosa mbalimbali nje ya majukumu yao rasmi humu nchini.
Hatua hii inaashiria kuwa Uingereza inapania kuimarisha uwajibikaji wa wanajeshi wake wanaohudumu katika mataifa ya nje.
Hayo yanajiri, huku Uingereza ikitetea uhusiano wake wa miaka mingi na Kenya kupitia mpango wa mafunzo kwa wanajeshi wake nchini Kenya (BATUK).
Wanajeshi hao wanaoishi katika kambi ya kikosi hicho iliyoko Kaunti ya Laikipia wamekuwa wakilaumiwa kwa mauaji tata, uharibifu wa mazingira na kuendeleza visa vya unyanyasaji wa kingono dhidi ya wenyeji.
Kwenye taarifa iliyowasilishwa kwa Kamati ya Bunge la Kitaifa Kuhusu Ulinzi na Mahusiano ya Kimataifa, Wizara ya Ulinzi ya Uingereza ilieleza mchango wa kiuchumi wa mpango wa BATUK nchini Kenya na manufaa mengine kwa nchi hizo mbili.
Kamati hiyo inayoongozwa na Mbunge wa Belgut Nelson Koech, wakati huu inaendesha uchunguzi kuhusu shughuli za BATUK nchini.
Wizara ya Ulinzi ya Uingereza pia ilielezea mageuzi yanayolenga kuzuia mienendo mibaya miongoni mwa wanajeshi wake walioko Kenya, huku familia za waathiriwa wa maovu yao kama vile Agnes Wanjiru na Tilam Leresh zikiendelea kutafuta haki.
Kenya imeanzisha mchakato wa unaolenga kufanikisha kurejeshwa Kenya kwa mwanajeshi anayetuhumiwa katika mauaji ya Bi Wanjiru mnamo 2012.
Shughuli hiyo inaweza kuchukua miezi kadhaa au hata miaka.
Hata hivyo, Uingereza imekubali kwamba wanajeshi waliotuhumiwa kwa uhalifu uliotenda nje ya majukumu yao rasmi wanaweza kuadhibiwa kwa mujibu wa sheria za Kenya na taratibu za mahakama.
“Kenya iko na haki ya kushughulikia maovu yote yanayodaiwa kutekelezwa na wanajeshi wa Uingereza dhidi ya Wakenya, isipokuwa maovu yaliyotendeka wakati wanajeshi hao wanaendesha majukumu rasmi,” Uingereza ilisema kwenye taarifa.
Ilirejelea Mkataba wa Ushirikiano wa Kijeshi kati ya Uingereza na Kenya wa 2015 (DCA) na uliofanyiwa marekebisho 2021.
Makubaliano hayo yanawapa wanajeshi wa Uingereza kinga fulani ya kidiplomasia wakiwa kazini.