Zaidi ya milioni 3 waanza mitihani Gredi 6, 9 kitaifa
MITIHANI ya kitaifa kwa wanafunzi zaidi ya milioni 3.4 kutoka shule za umma na za kibinafsi ilianza jana kote nchini. Mitihani hiyo inajumuisha ya wanafunzi wa Gredi ya Sita (KPSEA), Gredi ya Tisa (KJSEA) pamoja na KILEA na KPLEA kwa wanaofuata mtaala wa hatua za kujifunza.
Akisimamia usambazaji wa karatasi za mtihani katika Kaunti Ndogo ya Bureti, Kaunti ya Kericho, Waziri wa Elimu Julius Ogamba alihakikishia umma kuwa hatua madhubuti zimewekwa ili kulinda uadilifu wa mitihani.
Mwaka huu, jumla ya wanafunzi 3,428,729 wanafanya mitihani katika vituo 68,546 wakiwemo 1,298,089 (KPSEA), 1,130,669 (KJSEA), 2,414 (KILEA) na 1,479 (KPLEA).
KPSEA ni ya kuchagua majibu pekee, huku KJSEA ikiwa na maswali ya kuchagua na inayo hitaji majibu ya kuandikwa. Polisi watalinda tu mtihani wa KCSE, huku KPSEA na mitihani mingine ikisimamiwa na walimu na maafisa wa elimu.
Katika Kaunti ya Trans Nzoia, baadhi ya vituo vikiwemo Matisi Friends, Central Primary School, St John’s Education Centre, Linta Academy na Royal Victor vilipata mkanganyiko wa karatasi za mtihani. Mkurugenzi wa Elimu wa kaunti hiyo, Pamela Akello, alithibitisha tukio hilo, lakini akasema lilitatuliwa bila kuathiri uadilifu wa mtihani.
Aliongeza kuwa kuchelewa kuliathiri wanafunzi ambao hawakuhudhuria majaribio ya maandalizi. Trans Nzoia ina wanafunzi 24,312 wa KJSEA na 26,961 wa KPSEA katika shule za umma, na 23,097 wa KJSEA na 5,174 wa KPSEA katika shule binafsi. Shule za Kitale School na Mary Immaculate Primary ziliendelea vizuri na mitihani.
Katika Kaunti za Uasin Gishu na Baringo, mitihani ilianza chini ya ulinzi mkali. Katika Kaunti ya Uasin Gishu, Mkurugenzi wa Elimu David Koech alisema wanafunzi 10 wanafanya mitihani hospitalini jijini Eldoret, akiwemo mama mchanga na wengine waliotoka kaunti jirani.
Kamanda wa Polisi, Benjamin Mwanthi, alionya dhidi ya udanganyifu na kuwaonya polisi dhidi ya kubeba simu wakiwa kazini.
Katika Kaunti ya Baringo, mitihani ilianza bila matatizo katika vituo 756, na vifaa vikitolewa kutoka kontena 19. Dkt Kipruto Kosgei, ambaye ni Mkurugenzi wa Elimu wa kaunti hiyo, alisema kuna wanafunzi 15,672 wa KPSEA na 15,411 wa KJSEA. Hata shule zilizokuwa zimeathiriwa na mafuriko kama Noosukro na Loruk Primary, zimeshiriki mitihani hiyo. Ulinzi pia umeimarishwa kwa wadau wote.
Katika Kisumu Central, kontena ya mitihani ilifunguliwa saa kumi na mbili asubuhi na Naibu Kamishna wa Kaunti Langat Bosek. Mwenyekiti wa Baraza La Kitaifa La Mitihani Kenya (KNEC) Profesa Julius Nyabundi alisisitiza mabadiliko kutoka neno “mitihani” kwenda “tathmini” na kupunguza uwepo wa polisi shuleni ili kujenga uaminifu.
Katika Kaunti ya Kisii, mitihani ilianza vyema katika vituo vyote. Naibu Kamishna Joseph Mwangi anayesimamia Kisii Central na Nyaribari Chache, alisimamia usambazaji wa mitihani katika shule 78 za umma na 14 za binafsi.
Katika Kaunti ya Homa Bay, Mkurugenzi wa Taasisi ya Kitaifa ya Kukuza Mitaala (KICD) Prof Charles Ong’ondo alisema matokeo yatatangazwa kabla ya Sikukuu ya Krismasi. Alibainisha kuwa tathmini za mfumo wa CBE ni sehemu ya mabadiliko kutoka mfumo wa 8-4-4 na akawahimiza wazazi na walimu kuwa watulivu.
Aliongeza kuwa polisi watasimamia tu mtihani wa KCSE. Kamishna wa Kaunti Ronald Muiwawi alikiri kuwepo kwa udanganyifu zamani kuliweka doa katika mitihani ya kitaifa miaka ile, huku Mkurugenzi wa Elimu Eunice Khaemba akisema kuna wanafunzi 39,436 wa KPSEA na 36,496 wa KJSEA.
Katika Kaunti ya Siaya, kontena ilifunguliwa saa kumi na mbili asubuhi, na wakuu wa shule wakakusanya vifaa kwa wakati. Naibu Kamishna Robert Ngetich aliwataka wasimamizi na wanafunzi kuwa waadilifu, hasa ikizingatiwa kuwa huu ndio mtihani wa kwanza wa KJSEA.
Katika kaunti zote Kericho, Trans Nzoia, Uasin Gishu, Baringo, Kisumu, Kisii, Homa Bay na Siaya, serikali imesisitiza uzingatiaji wa sheria, uadilifu na usalama katika kuhakikisha mitihani ya kitaifa inafanywa kwa haki na uaminifu.