Msikiti wa Jamia kuandaa maonyesho ya historia ya miaka 100
MSIKITI wa Jamia katikati mwa jiji la Nairobi, ambao ndio mkongwe zaidi Afrika Mshariki, utafungua mlango wake leo kwa umma kutazama utajiri wake wa kihistoria na kujifunza mengi kuhusu dini ya Kiislamu.
Msikiti huo umewaalika Wakenya kufahamu mengi kuuhusu kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 100 tangu kuanzishwa kwake.
Kila anayetaka kufahamu historia pevu ya msikiti huo amealikwa kufika leo huku tamati ya shughuli yenyewe ikiwa ni Alhamisi.
Jana, Katibu Mkuu wa Jamia, Sheikh Abdulbari Hamid, alizindua hafla ya maonyesho ambapo picha za kale zilitolewa na kuwekwa kwa umma kutazama.
“Maonyesho hayo yatashirikisha picha za kale ambazo zilipigwa hata wakati ambapo jiwe la msingi la ujenzi lilikuwa likiwekwa miaka ya 20. Pia watafundishwa kuhusu msingi wa msikiti wa Jamia kielimu na kidini kwa Waislamu na nchi nzima,” akasema Bw Hamid.

Alikuwa akiongea kwenye kikao na wanahabari msikitini humo ambapo alifichua kuwa wakuu wa mashirika mbalimbali ya Kiislamu pamoja na maafisa wa serikali pia wamealikwa. Aliandamana na Imam wa msikiti huo, Sheikh Jamaldin Omar.
“Huu msikiti ulijengwa kwa muundo wa kipekee tena wa kale na hata kama umepanuliwa kukidhi idadi ya juu ya waumini, bado historia hiyo ipo,” akaongeza.
Wakati wa maonyesho hayo, uongozi wa msikiti huo pia utathmini hatua ambazo zimepigwa na pia juhudi zinazostahili kuongezwa kuhakikisha msikiti unawahudumia waumini wa Kiislamu.
Kwa sababu upo katikati mwa jiji, msikiti wa Jamia umekuwa ukiwapokea wageni hata wale kutoka nje ya nchi wanaozuru nchi kwa shughuli rasmi za serikali zao.