Mtawa aliyeshukiwa kuua mwenzake aachiliwa huru
MTAWA wa Kanisa Katoliki, Bi Caroline Kanjiru, ambaye alikuwa akizuiliwa na polisi kuhusiana na mauaji ya mwenzake, sasa atageuzwa kuwa shahidi wa serikali huku uchunguzi kuhusu kifo hicho ukiendelea.
Mtawa Anselimina Karimi, mwenye umri wa miaka 65, ambaye alikuwa msimamizi wa Kituo cha Watoto cha Meru, Nkabune, viungani kwa mji wa Meru, alipatikana akiwa amekufa nyumbani kwake mnamo Oktoba 12, 2025, damu ikitoka kichwani.
Baada ya tukio hilo, mahakama ya hakimu mjini Meru iliruhusu Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kumzuilia Dada Kanjiru kwa siku 14 katika Kituo cha Polisi cha Meru ili kuruhusu uchunguzi zaidi, ikiwemo kuchambua data za simu na kufanya uchunguzi wa DNA.
Hata hivyo, kesi ilipotajwa jana mahakamani, Bw Patrick Wachira, afisa wa uchunguzi kutoka makao makuu ya DCI, alieleza mahakama kuwa uchunguzi haujampata Mtawa Kanjiru na uhusiano wowote na mauaji hayo.
“Tulifanya uchunguzi wa mauaji, tukachambua rekodi za simu na kuhoji mashahidi. Baada ya uchunguzi huo, tumebaini kuwa mtuhumiwa hana uhusiano wowote na mauaji haya,” alisema Bw Wachira mahakamani.