Habari

Wakazi waishi na hofu mwili bila kichwa ukipatikana kijijini

Na DOMNIC OMBOK October 29th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAKAZI wa Kijiji cha Keiyo, Kaunti ya Kisumu, wanaishi kwa hofu baada ya mwili wa mwanaume bila kichwa kupatikana katika tukio linaloelezewa kuwa la kutisha na kikatili zaidi kuwahi kushuhudiwa eneo hilo.

Saa kumi na  mbili na nusu  asubuhi Jumanne, Wickliffe Okonjo, mwendesha bodaboda wa eneo la Achego, alikuwa akijiandaa kuanza kazi yake ya kila siku alipofahamishwa na mpita njia kuhusu gunia lililokuwa na damu ambalo lilikuwa limetupwa kando ya barabara.

“Yule mtu aliniambia ameona gunia lenye damu na akaniomba twende kuona. Tulipofika, tulishtuka kuona kichwa cha binadamu ndani ya mfuko wa karatasi,” alisema Bw Okonjo kwa mshtuko.

Okonjo alikimbilia kituo kidogo cha polisi cha Achego kutoa taarifa. Polisi walifika mara moja eneo la tukio katika barabara ya Achego–Muhoroni na kuthibitisha kuwa kichwa cha mtu kilikuwa kimetupwa barabarani ndani ya mfuko wa karatasi.

Wakiwa bado wanachunguza eneo hilo, polisi walipokea simu nyingine ya dharura kutoka kijiji jirani cha Keiyo, ambapo mwili usio na kichwa ulikuwa umepatikana karibu na boma moja katika eneo la Songor, tarafa ya Tamu.

Walipofika eneo hilo, walibaini kuwa si kichwa pekee kilichokuwa kimekatwa, bali pia sehemu za siri za marehemu. Baadaye, polisi walimtambua marehemu kuwa Patrick Okello, dereva wa trekta mwenye umri wa miaka 41, asili yake ikiwa ni kijiji cha Mawego katika Kaunti ya Homa Bay, lakini alikuwa akiishi Keiyo na mkewe pamoja na mtoto wao.

“Nimemjua Bw Okello kwa muda mrefu, alikuwa mtu mwema na hakuwa na ugomvi na mtu yeyote. Hatujui ni nani alifanya unyama wa namna hii,” alisema Bw Okonjo.

Kamanda wa Polisi wa Kaunti Ndogo ya Muhoroni, Fredrick Ombaka, alithibitisha tukio hilo akilitaja kuwa la kutisha na  kinyama zaidi kuwahi kushuhudiwa katika eneo hilo.

“Mwili ulipatikana karibu na nyumba yake ya kupanga. Kichwa na sehemu zake za siri zilikuwa zimekatwa,” alisema Bw Ombaka.

Aliongeza kuwa hakuna mtu aliyekamatwa kufikia sasa na kwamba uchunguzi unaendelea kubaini kilichotokea na waliohusika.

“Ni tukio la kutisha sana. Tunafanya uchunguzi wa kina ili kuwakamata waliohusika na kuhakikisha haki inapatikana,” aliongeza.

Tukio hilo limezua hofu na wasiwasi mkubwa miongoni mwa wakazi wa eneo hilo, wengi wao wakihofia huenda ni mauaji ya kisasi.

“Hatujawahi kuona jambo kama hili. Watu wanaogopa. Tunataka usalama urejeshwe na waliohusika wakamatwe,” alisema John Onyango, mkazi wa eneo hilo.

Mwili wa marehemu ulipelekwa hadi Hifadhi ya Maiti ya Othoo kwa uchunguzi wa maiti, huku polisi wakiahidi kuongeza doria kuimarisha usalama katika eneo la Muhoroni na vitongoji vyake.