Habari

Jinsi shirika la Global Fund linavyowainua vijana kaunti ya Machakos

Na SAMMY KIMATU October 30th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

WAJUMBE kutoka Global Fund walitembelea Kituo cha “Drop-In” Kaunti ya Machakos, ikiwa ni sehemu ya ziara maalum ya kukagua miradi inayofadhiliwa na shirika hilo na kuzungumza moja kwa moja na wanachama wake.

Ziara hiyo inalenga kutathmini maendeleo na changamoto wa miradi inayotekelezwa kwa kushirikiana na Benki la Dunia nchini Kenya.

Kituo hicho cha “Drop-In” kinasimamiwa na Deaf Empowerment Kenya (DEK) kwa ushirikiano na Serikali ya Kaunti ya Machakos, na kinahudumia vijana kwa kutoa huduma muhimu za ushauri nasaha, kutoa huduma za kupima virusi vya ukimwi, matibabu, pamoja na mafunzo ya ujasiriamali na ujuzi wa maisha.

Kituo hicho pia kinatambulika kama sehemu salama kwa vijana wote, wakiwemo wale wanaoishi na ulemavu.

Mkurugenzi wa DEK, Bw Joseph Ngari, aliishukuru Global Fund kwa kuendelea kufadhili miradi ya jamii inayolenga vijana na watu wanaoishi na ulemavu.

Aliahidi kuwa fedha na misaada inayotolewa itatumika kwa uadilifu mkubwa ili kufanikisha malengo yaliyowekwa.

“Asanteni kwa kuunga mkono mradi wetu. Tunaahidi kutumia fedha hizi kwa njia bora na yenye manufaa kwa jamii,” alisema Bw. Ngari.

Ujumbe huo uliokuwa na wabunge kutoka Bunge la Ujerumani ulipokelewa rasmi na Katibu wa Idara ya Jinsia na Ustawi wa Jamii wa Kaunti ya Machakos, Bi Bernardette Wavinya, ambaye alisifu Global Fund kwa mchango wake mkubwa katika sekta ya afya na ustawi wa kijamii.

Alisisitiza kuwa ushirikiano kama huo unasaidia serikali za kaunti kufikia malengo ya maendeleo endelevu.

Serikali ya Kaunti ya Machakos, chini ya uongozi wa Gavana Wavinya Ndeti, imeahidi kuendelea kushirikiana na wadau wa maendeleo katika kukuza afya, elimu, na ustawi wa kijamii.

“Milango yetu ipo wazi kwa washirika wa maendeleo wanaoshirikiana nasi katika ndoto ya kujenga jamii yenye uwezo wa kijamii na kiuchumi,” alisema Gavana Ndeti katika taarifa yake.

Gavana aliongeza kuwa ushirikiano kati ya serikali, mashirika ya kijamii, na wadau wa kimataifa kama Global Fund ni muhimu ni muhimu katika kubadilisha maisha ya wananchi, hasa vijana na makundi maalum.