Wanafunzi 17 wa Gredi ya sita wafanyia KPSEA hospitalini baada ya kujifungua
WANAFUNZI 17 wa Gredi la Sita wamefanyia mtihani wa Kenya Primary School Education Assessment (KPSEA) katika Hospitali ya Rufaa ya Nyambene, Kaunti ya Meru baada ya kujifungua.
Tukio hilo limeibua wasiwasi miongoni mwa wadau wa elimu na afya, kwani Meru inaendelea kuorodheshwa miongoni mwa kaunti zenye kiwango cha juu cha mimba za mapema na ukatili wa kijinsia (SGBV).
Kulingana na Daktari Githu Wachira, msimamizi wa matibabu katika hospitali hiyo, asilimia 49 ya wanawake waliojifungua mwezi Septemba walikuwa ni wasichana wa umri wa ujana.
Aidha, asilimia 70 ya visa vya matatizo wakati wa kujifungua vilirekodiwa miongoni mwa wasichana walio chini ya miaka 17.
“Hili ni janga kubwa kwa jamii. Tuna kina mama wachanga wenye umri wa miaka 12. Mbali na changamoto za kiafya, wanakumbana na unyanyapaa wa kijamii. Tunashirikiana na wadau wengine kuwasaidia kupitia ushauri na uangalizi,” alisema Dkt Wachira.
Daktari huyo aliongeza kuwa kuna haja ya ushirikiano wa pamoja kati ya wazazi, viongozi wa dini, walimu, wahudumu wa afya na maafisa wa utawala ili kupunguza visa vya mimba za mapema.
Hospitali ya Nyambene inaendesha mpango maalum wa kusaidia kina mama wachanga unaolenga kuwapatia ushauri, elimu ya malezi, na uhamasisho kuhusu namna ya kufikia ndoto zao licha ya changamoto walizonazo.
“Tunawasaidia kupitia elimu na ushauri nasaha ili waweze kujenga maisha bora. Pia tunalenga kuzuia hali ya kurudia kupata mimba kwa sababu baadhi yao tayari wana watoto watatu, jambo linaloongeza hatari za kiafya na kijamii,” aliongeza Dkt Wachira.
Takwimu kutoka idara ya afya ya Kaunti ya Meru zinaonyesha kuwa asilimia 24 ya wanawake wote wanaojifungua hospitalini ni wasichana vijana.
Kwa jumla, Kaunti ya Meru ina wanafunzi 31,785 wanaofanya mtihani wa KPSEA mwaka huu, 29,744 wa KJSEA na 31,620 wa KCSE.
Wadau wa elimu wameelezea hofu kuwa idadi kubwa ya wajawazito wa umri mdogo inaweza kuathiri malengo ya elimu ya wasichana na mustakabali wa maendeleo ya kijamii na kiuchumi katika eneo hilo.
Wameitaka serikali na jamii kuzingatia elimu ya afya ya uzazi shuleni, kuimarisha ushauri kwa vijana na kuhakikisha watuhumiwa wa mimba za mapema wanachukuliwa hatua kali za kisheria.