NACADA yanasa pombe feki ya thamani ya Sh5.28M, Kajiado
MAMLAKA ya Kitaifa ya Kupambana na Matumizi ya Pombe na Mihadarati (NACADA) imenasa pombe feki ya thamani ya Sh5.28 milioni katika operesheni iliyoendesha mjini Kitengela, Kaunti ya Kajiado.
Hii ni baada ya maafisa wa asasi hiyo, wakishirikiana na wale wa Mamlaka ya Ushuru Nchini (KRA) na Shirika la Kitaifa la Polisi (NPS) kuvamia duka la Scotland Wines and Spirits.
Wakati wa uvamizi huo, mmiliki wa duka hilo, ambaye anasemekana amekuwa akifuatwa na maafisa wa asasi hizo, alikamatwa.
Mshukiwa huyo aliwapeleka maafisa hao hadi katika konteina moja mjini Kitengela ambamo kulihifadhiwa katoni za pombe hiyo feki.
Jumla ya katoni 528 za aina mbalimbali za mvinyo zilipatikana katika konteina hiyo.
Hizo ni pamoja na; katoni 230 za mvinyo aina ya Trace Vodka, katoni 107 za Dalas Brandy, katoni 44 za Supa Vodka, katoni 22 za Rider Vodka, katoni 85 za Triger Gin na katoni 12 za mvinyo chapa Tiger Vodka.
Kila katoni ilibeba chupa 20 za mililita 250 kila moja.
Maafisa wa KRA walichukua shehena hiyo yote iliyosafirishwa hadi katika bohari lake lililoko Nairobi kwa uchunguzi zaidi.
Maafisa kutoka Shirika la Kukadiria Ubora wa Bidhaa Nchini (KEBS) walikusanya sampuli kadhaa kufanyiwa uchunguzi wa maabara kubaini kiwango cha ubora sawa na hatari yake kwa afya ya umma.
Afisa Mkuu Mtendaji wa NACADA Anthony Omerikwa alisema operesheni hiyo ilitokana na agizo lililotolewa na Waziri wa Usalama Kipchumba Murkomen kuhusu kuangamizwa kwa pombe haramu.