Ushindi kwa Inspekta Jenerali korti ikisema ndiye mwajiri wa polisi
MAHAKAMA ya Ajira na Mahusiano ya Kazi imeamua kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi Douglas Kanja ndiye pekee mwenye mamlaka ya kuajiri, kupandisha vyeo na kushughulikia nidhamu ya maafisa wa Huduma ya Kitaifa ya Polisi (NPS).
Uamuzi huo unafungua njia kwa mchakato wa kusajili makurutu 10,000 wa polisi kuendelea bila vikwazo, chini ya uongozi wa Bw Kanja.
Jaji Hellen Wasilwa, katika uamuzi wake, alisema mamlaka ya Inspekta Jenerali wa Polisi yamehakikishwa na Katiba chini ya Ibara ya 245(1) na (2)(b), na hakuna mtu au shirika lolote, ikiwemo Tume ya Huduma ya Polisi (NPSC), inaweza kuelekeza au kuingilia majukumu yake.
Aidha, Jaji Wasilwa alitoa amri inayokataza NPSC kuingilia mchakato wa usajili wa makurutu wa polisi 10,000 uliotangazwa mwezi uliopita, akisema jukumu hilo liko chini ya mamlaka ya moja kwa moja ya NPS.
“Korti imepiga marufuku NPSC kuingilia ajira ya maafisa wa polisi kwa kuwa jukumu hilo ni sehemu ya majukumu ya kiutendaji ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi,” alisema Jaji Wasilwa.
Uamuzi huo umetuliza mvutano wa muda mrefu kati ya ofisi ya Inspekta Jenerali na NPSC, ukithibitisha uhuru wa ofisi ya Bw Kanja huku ukibainisha jukumu la tume hiyo kuwa la kiutawala pekee.
Kesi hiyo iliwasilishwa na aliyekuwa mbunge wa Kilome Harun Mwau mnamo Septemba 30, 2025, akipinga mamlaka ya NPSC katika usajili wa maafisa wa polisi.
Bw Mwau alidai vitendo vya tume hiyo vinakiuka Katiba na akaomba mahakama ibatilishe baadhi ya vifungu vya Sheria ya Tume ya Huduma ya Polisi na Sheria ya Huduma ya Kitaifa ya Polisi.
Alisisitiza kuwa uajiri unapaswa kufanywa na Huduma ya Polisi chini ya amri ya moja kwa moja ya Inspekta Jenerali, kwa mujibu wa Ibara za 238, 239 na 245 za Katiba.
“Huduma za usalama wa taifa lazima ziakisi utofauti wa Wakenya, na jukumu hili haliwezi kuhamishwa kikatiba kwa tume yoyote,” alisema.
