Habari

Bei ya koti za wanaume yapanda kwa kasi zaidi nchini- ripoti

Na DOMNIC OMONDI November 1st, 2025 Kusoma ni dakika: 2

BEI ya koti za wanaume imepanda kwa kasi zaidi katika sekta ya nguo na viatu kati ya Septemba na Oktoba 2025, licha ya bei ya jumla ya bidhaa nchini kubakia bila mabadiliko mwezi Oktoba.

Takwimu kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS) zinaonyesha kuwa bei ya koti za wanaume ilipanda kwa asilimia 4.6 katika kipindi cha miezi miwili, ikiwa ndio ongezeko kubwa zaidi miongoni mwa bidhaa zote zilizoorodheshwa katika kundi la nguo.

“Septemba hadi Oktoba 2025, bei za nguo zilionyesha mabadiliko mseto. Bei za suti za wanaume na sare za wasichana zilipungua kwa asilimia 0.1 kila moja. Kwa upande mwingine, bei ya koti za wanaume iliongezeka kwa asilimia 4.6, huku mashati ya wanaume yakipanda kwa asilimia 0.3,” taarifa ya KNBS ilisema.

Kupanda huko kwa bei kunahusishwa na mchanganyiko wa sababu za hali ya hewa na msimu wa utalii. Mvua fupi nchini Kenya huanza Oktoba hadi Desemba, kipindi ambacho pia kinaambatana na msimu wa kilele cha utalii. Asubuhi na jioni huwa na baridi kali, hivyo kuongeza mahitaji ya mavazi ya joto kama koti.

Watalii wanaozuru maeneo ya juu kwa safari za maporini pia huongeza mahitaji ya koti.

Kwa ujumla, kiwango cha mfumko wa bei nchini kilibakia asilimia 4.6 sawa na Septemba, kwani ongezeko la bei za bidhaa zisizo za chakula na mafuta lilibatilisha upungufu wa bei za chakula na usafiri.

Katika kipindi cha miezi 12 hadi Oktoba 2025, bei katika kitengo cha nguo na viatu ziliongezeka kwa asilimia 2.9, zikichochewa zaidi na mahitaji makubwa ya koti ya wanaume.

Utafiti wa kimataifa wa Statista unakadiria kuwa mapato katika soko la mavazi nchini Kenya mwaka 2025 yatafikia dola bilioni 6.19 (Sh802 bilioni), huku mavazi ya wanawake yakiongoza kwa thamani ya dola bilioni 2.33 (Sh302 bilioni).

Shirika la KNBS hukusanya takwimu hizi kupitia utafiti wa kila mwezi wa bei katika maeneo 50 ya mijini nchini, kati ya wiki ya pili na ya tatu ya kila mwezi.

Mfumko wa bei umesalia ndani ya kiwango kinachokubalika na Benki Kuu ya Kenya cha kati ya asilimia 2.5 na 7.5, huku watunga sera wakielekeza nguvu zao katika kukuza uchumi na kuongeza ajira.

Kwa sasa, thamani ya shilingi ya Kenya imesalia thabiti, ikibadilishwa kwa wastani wa Sh129 kwa dola moja ya Amerika katika kipindi cha mwaka uliopita.