Malumbano makali katika uchunguzi wa kifo cha Rex Masai
MALUMBANO makali yalizuka kortini Oktoba 30,2025 katika uchunguzi wa kubaini kilichosababisha kifo cha mwanaharakati Rex Masai Juni 20 2024 baada ya ombi kuwasilishwa Naibu Inspekta Jenerali (DIG) Eliud Langat afike kortini kutoa ushahidi.
Maandamano hayo ya Gen Z yalikuwa yanapinga Sheria ya Fedha 2024/2025.
Zaidi ya watu 60 waliuawa na polisi wakati wa maandamano hayo.
Mawakili wa mamlaka huru ya polisi (IPOA), afisi ya mkurugenzi wa mashtaka ya umma (DPP) na wale wa Huduma ya Polisi (NPS) walikabiliana vikali mbele ya hakimu mwandamizi Geoffrey Onsaringo anayeongoza uchunguzi huo.
Cheche za maneno makali , shutuma na lawama za kujaribu kuficha ukweli zilitanda.
Mawakili wa IPOA na DPP walitaka Langat aagizwe afike kortini kueleza kuhusu ya barua aliyoandika kuhusu kutokuwapo kwa mpango na utaratibu wa kudhibiti maandamano kupinga sheria ya fedha ya 2024/2025 yaliyoongozwa na Gen Z.
Wakili wa NPS alipinga hatua ya kumtaka Langat afike kortini na kuilaumu IPOA kwa kujaribu kuficha ukweli ukisemwa.
“IPOA na DPP wanajaribu kuficha ukweli katia uchunguzi kwa kukataa kuwaita mashahidi 10 walioandikisha taarifa na samanzi zao kufika kortini kutolewa,” mawakili wa NPS walifichua.
Baadhi ya ushahidi ambao haujawasilishwa kortini ni pamoja na ule George Ndikas aliyekuwa akitembea na marehemu Rex Masai mnamo Juni 20,2024.
IPOA ilisema kuna barua ya DIG Langat kuhusu maandamano hayo nayo pia haijatolewa kama ushahidi.
Kufuatia ufichuzi huo mawakili wa DPP, NPS na IPOA walilumbana vikali hata ikabidi hakimu aahirishe kikao na kuwapa muda wanasheria hao kuafikiana ikiwa DIG Langat atafika kortini au la pamoja na idadi ya mashahidi waliosalia.
“Ushahidi wote unatakiwa kuwasilishwa kortini na DPP. Pia naomba hii mahakama imwamuru DPP afike kortini aeleze masuala Fulani kuhusu mauaji haya,” wakili Moses Kipkogei wa NPS alisema.
Baada ya muda wa zaidi ya nusu saa wa majimbizano makali, mawakili hao waliafikiana.
Waliambia korti, “tumekubaliana DIG Langat asifike kortini lakini aliyekuwa naibu wa kamanda wa polisi kaunti ya Nairobi Doris Mugambi afike kortini kujibu maswali.”
Bi Mugambi ndiye alikuwa anasimamia vikosi vya polisi vilivyokuwa vinadhibiti usalama na kulinda mali na biashara wakati wa maandamano hayo yaliyopelekea watu zaidi 60 kuuawa miongoni mwao Rex.
Pia mawakili hao walikubaliana mashahidi 10 waitwe kabla ya uchunguzi huo kufungwa.
Mawakili wa NPS walimkashfu DPP kwa kutoeleza sababu za kutowaita mashahidi hao 10 ilhali walikuwa wametambuliwa na kuandika taarifa kwa IPOA.
NPS ilisema mashahidi muhimu ni , Ndikas , Dkt Lawrence Machira ambaye alimwona mara ya mwisho Rex akiwa hai na afisa wa DCI Tiberius Ekisa.
Mawakili hao wa NPS Moses Kipkogei na Elias Ouma waliomba DPP Renson Ingonga mwenyewe afike kortini kueleza sababu ya kuagiza IPOA kuchunguza mauaji hayo ya Rex baada ya masaa 12, Juni 21,2024.
“Naomba hii mahakama iamuru DPP mwenyewe afike kortini kufafanua sababu ya kuamuru IPOA kuchunguza mauaji ya Rex badala ya kuagiza idara ya uchunguzi wa jinai (DCI) kuchunguza mauaji hayo,” Bw Kipkogei alimweleza hakimu.
Wakili huyo alisema DPP anatakiwa kueleza sababu ya kufikiria Rex aliuawa na afisa wa Polisi.
“Ni jambo la kutamausha DPP kufikiri Rex aliuawa na afisa wa polisi. Naomba hii mahakama imwamuru DPP afike kortini mwenyewe kueleza sababu alifikia uamuzi Rex aliuawa na afisa wa polisi,” Bw Kipkogei alisema.
Maafikiano ya kuwaita mashahidi 10 zaidi kuliathiri kutofungwa kwa uchuguzi huo ambao familia ya Rex Masai ilieleza kortini umechukua zaidi ya miezi 12 kukamilishwa.
Uchunguzi huo ulikuwa ukamilishwe Oktoba 30,2025 lakini ukakwama baada ya ombi la DIG Langat afike kortini.
Uchunguzi huo uliahirishwa hadi Novemba 11,2025.