Minara ya Kemboi, Vivian kuzinduliwa mjini Eldoret
Na MWANDISHI WETU
MINARA ya mabingwa wa Riadha za Dunia na Mbio za Olimpiki, Ezekiel Kemboi na Vivian Cheruiyot itazinduliwa mjini Eldoret mnamo Ijumaa, siku moja kabla ya mashindano ya Kitaifa ya Mbio za Nyika kuandaliwa katika uwanja wa Eldoret Sports Club.
Minara hiyo ambayo imeandaliwa na Hospitali ya Mediheal itazinduliwa katika makutano ya Barabara ya Nairobi-Kapsabet na Kaptagat.
Kemboi ameibuka mshindi wa Olimpiki katika mbio za mita 3,000 kuruka maji na viunzi mara mbili na kutawazwa mfalme wa dunia mara nne. Kwa upande wake, Cheruiyot alinyanyua nishani ya dhahabu katika mbio za mita 5,000 kwenye Olimpiki za Rio mnamo 2016. Wawili hao ni miongoni mwa wanariadha wanne ambao minara yao itazinduliwa kwa pamoja.
Cheruiyot ambaye kwa sasa amehamia kushiriki mbio za marathon, alitawazwa pia malkia wa Riadha za Dunia katika mbio za mita 5,000 mnamo 2009 na 2011 kabla ya kunyakua medali za dhahabu katika mbio za mita 10,000 kwenye Riadha za Dunia mnamo 2011 na 2015.
Katibu wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) katika eneo la Central Rift, Kennedy Tanui amefichua kwamba Rais wa AK, Jackson Tuwei atakuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo ya uzinduzi.
Kwa mujibu wa Tanui, wanariadha wote watakaoshiriki Mbio za Kitaifa za Nyika mwishoni mwa wiki hii, wanatakiwa kuwa mjini Eldoret kufikia Alhamisi.
Mkutano utakaowahusisha mawakala na makocha wa wanariadha utafanyika mnamo kesho katika hoteli ya Noble kabla ya semina ya wakimbiaji kuandaliwa katika eneo lilo hilo mnamo Ijumaa asubuhi.
Hii ni mara ya kwanza kwa mbio za nyika katika kiwango cha kitaifa kuandaliwa nje ya jiji la Nairobi. Uwanja wa Kipchoge Keino mjini Eldoret ulitumiwa kuandalia mchujo wa vikosi vilivyopeperusha bendera ya Kenya kwenye Olimpiki za Rio 2016 huku jiji la Mombasa likiwa mwenyeji wa mbio za nyika duniani mnamo 2007.
Mbio za kitaifa za nyika wikendi hii zitatumiwa pia kuteulia kikosi kitakachowakilisha Kenya katika Mbio za Dunia za Nyika (World Cross Country Championships) zitakazoandaliwa jijini Aarhus, Denmark mnamo Machi 30.
“Maandalizi kwa mchujo wa kitaifa wa mbio za nyika yamekamilika. Tunawasihi Wakenya kufika kwa wingi mjini Eldoret kushuhudia mojawapo ya mashindano ya haiba kubwa kuwahi kuandaliwa katika eneo zima la Bonde la Ufa,” akasema Tanui.