Familia ya Jaramogi yamsamehe Kahiga
FAMILIA ya Jaramogi Oginga Odinga imetangaza kuwa imemsamehe Gavana wa Nyeri Mutahi Kahiga kutokana na matamshi yake yaliyofasiriwa kuwa ya kusherehekea kifo cha aliyekuwa Waziri Mkuu Raila Odinga.
Seneta wa Siaya Dkt Oburu Oginga alisema kuwa wamemsamehe Bw Kahiga na gavana huyo yuko huru kufika Kang’o ka Jaramogi ila lazima aonyeshe kwamba amesikitikia kauli tata aliyotoa.
Akizungumza kwenye runinga ya NTV, Dkt Oginga ambaye pia ni kiongozi wa ODM, alisema kuwa hawana kinyongo wala kisasi na Bw Kahiga.
“Matamshi yake hayakunikasirisha kwa sababu ni ya kitoto. Ni matamshi kutoka mtu mdogo na ukiyashikilia rohoni basi moyo unaweza kukomesha mdundo wake hata kabla ya wakati wako utimie jinsi alivyopanga Mwenyezi Mungu,” akasema Dkt Oginga.
Bw Kahiga alinukuliwa akisema kuwa mauti ya Raila, 80, yaliyotokea Oktoba 15, 2025 akipokea matibabu India, yalikuwa baraka kwa watu wa Mlima Kenya.
“Ilikuwa mbinu ya Mwenyezi Mungu ya kuhakikisha kuwa serikali inawazia upya hatua yake ya kupeleka rasilimali za umma Luo Nyanza. Itafanya serikali itathmini hatua yake na kuzingatia mgao wa Mlima Kenya serikalini,” akasema Bw Kahiga katika mazishi moja eneobunge la Kieni.
“Hakuna aliyepigwa marufuku kufika Kangó ka Jaramogi kuomboleza nasi akiwemo Bw Kahiga kama ataomba msamaha. Kama anataka kuja kuomboleza nasi, nimemruhusu,” akaongeza Dkt Oginga.
Aliongeza kuwa kama familia ya Jaramogi hawamakinikii adui na mtu yeyote bali la muhimu ni kupalilia urafiki na wote.
Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Agikuyu Wachira Kiago alimshukuru Dkt Oginga akisema kuwa ameongozwa na hekima kumsamehe Bw Kahiga.
Alikiri kwamba matamashi ya Bw Kahiga yalikuwa yameongeza uhasama kati ya Mlima Kenya na familia ya Jaramogi.
“Hekima ya Dkt Oginga inaonyesha msamaha ambao pia ulikuwa kwa Raila. Ameonyesha kuwa hamakinikii masuala ambayo hayana maana na anamakinikia maridhiano,” akasema Bw Kago.