Viongozi wasusia kuapishwa kwa Suluhu
RAIS wa Tanzania Samia Suluhu jana aliwalaumu watu kutoka nje kwa kuhusika na maandamano ya kupinga kuandaliwa na pia matokeo ya uchaguzi huku akitoa wito wa umoja kwa sababu ya udhabiti wa nchi.
Akizungumza wakati wa kuapishwa kuhudumu muhula wa pili, Samia alisikitikia vurugu zilizotokea Tanzania akitoa wito kwa umma kudumisha amani na kumakinikia ujenzi wa taifa hilo.
“Haishangazi kuwa wale ambao walikamatwa wanatoka mataifa ya nje,” akasema bila kutoa ufafanuzi zaidi. Hii ilikuwa mara ya kwanza alikuwa akihutubu baada ya kuapishwa kufuatia matokeo ya uchaguzi huo.
“Kilichofanyika hakionyeshi tabia, tamaduni au malengo yetu kama raia wa Tanzania. Si ‘Utanzania. Haishangazi kuwa baadhi ya vijana walionyakwa kwa kushiriki ghasia si raia wa kigeni,
“Vyombo vyetu vya ulinzi na usalama vinaendelea kufanya uchunguzi ili kuhakikisha Tanzania inarejelea amani ambayo imezoeleka,” akasema.
Samia,65 na makamu wa rais Emmanuel Nchimbi waliapishwa na Jaji Mkuu Ibrahim Hamis Juma chini ya ulinzi mkali kufuatia uchaguzi ambao uligubikwa na maandamano na pingamizi za upinzani.
Uapisho huo uliandaliwa katika eneo la kijeshi jijini Dodoma badala ya uwanja jinsi ambavyo imekuwa ikifanyika katika miaka ya nyuma.
Umma haukuruhusiwa kuhudhuria sherehe hiyo ambayo ilipeperushwa mbashara kwenye runinga ya serikali.
Samia alitangazwa mshindi mnamo Jumamosi kwa asilimia 98 za kura. Alikuwa na upinzani mdogo kwa sababu ya viongozi wa upinzani na vyama vyao kuzuiwa kuwa na wagombeaji au kushiriki uchaguzi huo.
Waangalizi wa uchaguzi huo walitilia shaka uwazi wake kutokana na mauaji yaliyotokea ya waandamanaji wakati wa kura hiyo.
Bado haifahamiki idadi ya watu ambao wameuawa kutokana na ghasia ambazo zilitokea baada ya uchaguzi huo wa Oktoba 29. Wanajeshi walitumwa kuzima ghasia hizo huku Intaneti ikizimwa na imekuwa ikirejeshwa na wakati huo huo kukatizwa tangu kura hiyo.
Jana, Samia aliahidi kulinda amani na uhuru wa Tanzania kwa njia yoyote ile na kwa gharama yoyote.
“Marais wa Zambia na Burundi wametoa maoni yao kuhusu suala hili. Ghasia zinazoshuhudiwa nchini si nzuri na hazina thamani ya kuigwa. Kwa hivyo ndugu zangu nawaomba tudumishe amani na umoja kwa ajili ya nchi yetu,” akasema.
“Nataka kuchukua nafasi hii kuwaonya wale ambao walichochea maandamano na kuvuruga amani,” akasema.
Viongozi wa ukanda wa Jumuiya ya Afrika Mashariki jana walisusia sherehe hiyo ambayo iliratibishwa haraka na pia haikuchukua muda kama zile za zamani.
Ni marais watatu tu pekee waliohudhuria wakiwa Hakainde Chilema wa Zambia, Evariste Ndayishimiye wa Burundi na Sheikh Hassan Mahamud wa Somalia.
Nchi nyingine ziliwakilishwa na maafisa wa ngazi ya juu serikalini pamoja na mabalozi.
Kenya iliwakilishwa na Naibu Rais Profesa Kithure Kindiki nayo Jesica Alupo, makamu wa rais wa Uganda, akimwakilisha Rais Yoweri Museveni.
Marais wengi wa EAC walichelea kumpongeza kwa ushindi wake wakati ambapo matokeo yalitolewa Jumamosi. Ni wakati wa kuapishwa kwake ndipo Rais Ruto na Rais Museveni walimpongeza rasmi.
“Natao wito kwa raia wa Jamuhuri ya Tanzania wadumishe amani na kufuata sheria. Pia naomba viongozi wote waeneze amani na kukumbatia mazungumzo kuhusu utata wowote uliopo kwa ajili ya umoja wa nchi,” akasema Rais Ruto ambaye pia ni mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika Mahmoud Youssouf alijipata pabaya mitandaoni kwa kuharakisha kumpongeza Samia kwa ushindi wake baada ya kuzuka kwa ripoti ya kuuawa kwa waandamanaji.