Michezo

Kenya kuandaa mashindano ya kimataifa ya mpira wa vikapu ya wanawake, wanaume mwezi huu

Na GEOFFREY ANENE November 4th, 2025 Kusoma ni dakika: 2

KENYA imechaguliwa kuwa mwenyeji wa mashindano mawili makubwa barani Afrika ya mpira wa vikapu ya wanawake (WBLA) na wanaume (Road to Basketball Africa League Elite 16) jijini Nairobi.

Mashindano hayo mawili muhimu yanaashiria hatua kubwa katika safari ya michezo ya Kenya, yakidhihirisha hadhi yake inayoongezeka katika mpira wa kikapu barani Afrika.

Shirikisho la Mpira wa Vikapu Kenya (KBF) lilitangaza habari hizo Alhamisi, likieleza kuwa heshima ya kuwa mwenyeji ni “tukio la kihistoria” katika uongozi wa Kenya unaokuwa kwenye mchezo huo barani. “Mashindano haya mawili mfululizo ni hatua ya kihistoria katika ukuaji wa uongozi na ushawishi wa Kenya ndani ya mpira wa vikapu wa Afrika,” akasema Katibu Mkuu wa KBF, Angela Luchivya.

Mashindano ya WBLA yataanza Novemba 9–15, 2025, katika Ukumbi wa Nyayo. Yatahusisha klabu bora za wanawake kutoka Kanda ya Tano zikiwemo Halmashauri ya Bandari za Kenya (KPA) na Chuo Kikuu cha Zetech (Kenya), REG na APR (Rwanda), Fox Divers (Tanzania), Gladiators na Hippos (Burundi), pamoja na Magic Stormers (Uganda). Mashabiki wanatarajiwa kushuhudia mchezo wa kasi, umahiri, na ubabe unaoongezeka wa mpira wa vikapu wa wanawake katika ukanda huu.

Baada ya hapo kivumbi cha kinadada, macho yataelekezwa kwa Road to BAL Elite 16 mnamo Novemba 18–23, 2025, katika Ukumbi wa Kasarani. Mashindano hayo ya wanaume yatakutanisha klabu bora kutoka kote barani zikigombea nafasi za kufuzu kushiriki katika BAL ambayo ni ligi kuu ya kitaaluma ya Afrika inayoratibiwa kwa ushirikiano na FIBA na NBA.

Mabingwa wa Kenya, Nairobi City Thunder, watawakilisha taifa. Wanatarajiwa kuonyesha ubabe wao tena baada ya kuvutia mwaka 2024.

Uenyeji wa mashindano hayo mawili unathibitisha hadhi ya Kenya kama ngome ya mpira wa vikapu katika ukanda huu, huku yakionyesha vipaji vya ndani na kuimarisha mshikamano wa michezo barani. KBF imeshukuru Shirikisho la Mpira wa Vikapu barani Afrika (FIBA Africa) na Serikali ya Kenya kwa msaada wao endelevu, na ikatoa wito kwa wadhamini, washirika, na mashabiki kuunga mkono hafla hizi.

“Huu ni wakati wetu wa kuonyesha ulimwengu kwamba Kenya inaweza kuandaa mashindano ya kiwango cha juu,” aliongeza Luchivya. “Kwa pamoja, tunaweza kuhamasisha kizazi kijacho cha wachezaji na mashabiki, na kusherehekea roho ya umoja wa mpira wa kikapu wa Afrika.”