Idadi kubwa ya waliofariki kutokana na maporomoko ya ardhi ni watoto- katibu
IDADI kubwa ya watu ambao wamedhibitishwa kuaga dunia kutokana na maporomoko ya ardhi katika eneo la Chemororch kaunti ya Elgeyo Marakwet ni watoto wa umri wa kati ya miaka miwili na 17.
Katibu katika wizara ya elimu, Julius Bitok, alielezea masikitiko yake kuhusiana na vifo hivyo haswa vya watoto.
Bw Bitok alisema vifo hivyo vinahusu wanafunzi kutoka shule nane katika kaunti ndogo ya Kerio Valley.
Katibu huyo alifichua kuwa watoto wengi wangali hawajulikani waliko baada ya Kijiji hicho kusombwa na maporomoko ya ardhi.
“Jamii ya eneo hili imeachwa na uchungu mwingi kutokana na maafa haya hasa idadi kubwa ya watoto ambao wamefariki huku wengine wakiwa hawajapatikana,” alisema Bw Bitok.
Bw Bitok alisema watoto 15 ni kati ya watu 32 waliodhibitishwa kufariki kutokana na mkasa huo.
Juhudi zakutafuta watoto zaidi ambao hawajulikani waliko zinaendelea huku familia husika zikiendelea kusononeka kutokana na mkasa huo.
Bw Bitok alisema serikali kwa ushirikiano na mashirika ya misaada za kibinadamu inaendelea na juhudi za pamoja kusaidia familia ambazo zimeathirika.
Shirika la msalaba mwekundu linaendelea kuwapa chakula na misaada mingine ya kibinadamu huku serikali ikiahidi kugharamia gharama ya mazishi.
“Ni uchungu kwamba kufikia sasa ni watoto 15 ambao wameripotiwa kufariki kutokana na janga hili.Hata hivyo serikali inashirikiana na wadau wengine ili kusaida familia zilizoathiriwa mbali na serikali kujitolea kugharamia mahitaji ya mazishi kwa familia zote,” alisema Bw Bitok.
Mbali na misaada ya kibinadamu serikali imeweka mikakati ya kutosha ili kuona kuwa wahasiriwa wanapata ushauri nasaha ili kukabiliana na athari za janga hilo.