Mashujaa wa Mau Mau waishtaki serikali wakitaka fidia ya Sh10B
WALIOKUWA wapiganaji wa Mau Mau kutoka Kaunti ya Meru wameishtaki Serikali, wakitaka fidia ya Sh10 bilioni kwa vitendo vya ukiukaji wa haki walivyotendewa baada ya Kenya kupata uhuru.
Wakili Tom Macharia, anayewakilisha walalamishi hao, waliambia mahakama kwamba wanataka pesa hizo zilizopasa kutolewa kupitia Hazina ya Haki iliyopendekezwa na Rais Mstaafu Uhuru Kenyatta mnamo 2015.
“Wakati wa Hotuba yake kwa Taifa mnamo 2015, Rais Kenyatta aliomba msamaha kwa wapiganaji uhuru wote. Aliagiza kuundwa kwa Hazina ya Haki na kanuni kuhusu kuundwa kwake zilitayarishwa na Mwanasheria Mkuu,” wakili Macharia akaambia mahakama.
Mashujaa hao wa Mau Mau pia wanaitaka mahakama kuagiza utekelezaji wa mapendekezo ya Tume kuhusu Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC) ili kutoa haki na maridhiano kwa wapiganaji wa Mau Mau na familia zao.
Wameishtaki serikali kupitia Afisi ya Mwanasheria Mkuu na Tume ya Kitaifa ya Kutetea Haki za Kibinadamu.
Mahakama Kuu iliwasilisha kesi hiyo kwa Jaji Mkuu ili ateue jopo la majaji kuisikiza na kutoa uamuzi.
Katika agizo lake, Jaji Heston Nyaga alisema kuwa kesi hiyo inaibua masuala mazito ya kikatiba “yanayoathiri maelfu ya wapiganaji wa uhuru nchi Kenya na hivyo inafaa kusikizwa na jopo la majaji.”
Hata hivyo, Jaji huyo aliruhusu mawakili wa walalamishi kuchapisha kesi hiyo katika gazeti moja la kitaifa ili kuruhusu ushirikishaji wa watu wenye haja.
Jaji Nyaga aliamuru walalamishi kuweka tangazo hilo katika sehemu ya gazeti ambapo litaonekana wazi, ndani ya siku 21. Aidha, aliwaagiza wahusika kujiwasilisha kortini kwa ajili ya kusikizwa kwa kesi hiyo siku 21 baada ya tangazo la kesi hiyo kuchapishwa magazetini.
“Maagizo zaidi yatasubiriwa kutoka kwa afisi ya Jaji Mkuu. Kesi hiyo itatajwa na maagizo kutolewa mnamo Februari 9, 2026,” Jaji Nyaga aliamuru.
Kesi hiyo imewasilishwa na jumla ya waliokuwa wapiganaji wa uhuru 30 na jamaa za mashujaa wa Mau Mau na shirika lisilo la kiserikali la African Centre for Corrective and Preventive Action (ACCPA).