Wakenya wanaosaka ajira ng’ambo wafaa wajihadhari
KULINGANA na matokeo ya kura ya maoni yaliyotolewa na kampuni ya utafiti ya Infotrak, na kuchapishwa na gazeti hili Septemba 27, 2025, ukosefu wa ajira uliibuka kama mojawapo ya changamoto kubwa inayowasibu Wakenya wengi.
Kwa mujibu wa matokeo hayo, asilimia 73 ya Wakenya 2,400 waliohojiwa katika utafiti huo, wengi wao wakiwa vijana, wanahisi kuwa serikali inapaswa kutekeleza mikakati ya kupunguza kero hili.
Ingawa serikali ya Kenya Kwanza imeanzisha mipango mbalimbali ya kushughulikia ukosefu wa ajira miongoni mwa vijana, inaonekana haijafaulu kikamilifu.
Hii ndio, kwa mfano, bado kunaripotiwa visa ambapo baadhi ya Wakenya wanahadaiwa na kusajili katika jeshi la Urusi na kutumwa kupigana nchini Ukraine.
Ndio, Wakenya huhadaiwa kwa sababu ahadi wanazopewa na mashirika husika ni za nafasi za ajira katika kampuni kubwa nchini Urusi wala sio kujiunga na jeshi la nchi hiyo.
Mwezi jana, wa Oktoba, Mkuu wa Mawaziri na Waziri wa Masuala ya Kigeni Musalia Mudavadi aliungama kuwa kuna Wakenya waliosajiliwa katika jeshi la Urusi, kinyume na matakwa yao.
Ilidaiwa kuwa kuna baadhi yao ambao wanazuiliwa kama wafungwa kwa kivita nchini Urusi.
Mfano ni mwanariadha Evans Kibet, ambaye madhila yake yaliangaziwa na Shirika la Habari la Uingereza (BBC) mnamo Septemba 22, mwaka huu.
Kibet alisajiliwa nchini Kenya na kampuni fulani kwa ahadi kwamba angepewa ajira katika kampuni moja kubwa nchini Urusi, lakini ahadi hiyo haikutimizwa.
Nimetoa maelezo hayo kuweka msingi wa onyo langu kwa Wakenya, na haswa vijana, kwamba wajihadhari zaidi wanapojisajili na kampuni zinazoahidi kuwasaidia kupata ajira mataifa ya ng’ambo.
Kabla ya kukubali kusajiliwa na kampuni yoyote ile, wahakikishe kuwa kampuni husika ni halali na imeidhinisha na serikali kupitia Wizara ya Leba.
Wahakikishe kwamba jina la kampuni inayowasajili ni miongoni mwa majina ya kampun zilizoorodheshwa katika Mamlaka ya Kitaifa ya Uajiri (NEA).
Mnamo Januari mwaka huu, Waziri wa Leba Alfred Mutua aliwaonya Wakenya kuhusu sakata hii ya kampuni feki zinazowahadaa kuhusu nafasi za ajira ng’ambo ili wasije wakajipata wanapelekwa utumwani katika mataifa ya ng’ambo.
Kampuni hizi zilichipuza baada ya Serikali ya Kenya Kwanza kunzisha mpango maalum wa kuwasaidia Wakenya kupata ajira katika mataifa ya nje.
Chini ya mpango huo, serikali kupitia Wizara ya Leba na ile ya Masuala ya Kigeni zimekuwa zikitia saini mikataba ya ajira na nchi kadhaa za Kiarabu, Canada, Ujerumani, miongoni mwa nchi zingine.
Kulingana na Rais William Ruto, chini ya mpango huo, serikali yake inalenga kuhakikisha kuwa jumla ya zaidi ya Wakenya 400,000 wanapata ajira katika nchi za nje. Kupitia mpango huo, kiwango cha pesa zinazotumwa nchini na Wakenya wanaofanya kazi ughaibuni itaongezeka.
Kulingana na takwimu kutoka Shirika la Kitaifa la Takwimu (KNBS), Wakenya walioko ng’ambo walituma nyumbani jumla ya Sh350 bilioni katika mwaka wa 2024, pesa ambazo ziliwekezwa katika miradi mbalimbali yenye manufaa.
Kwa hivyo, huku Wakenya wakiwa na hamu ya ajira katika nchi za ng’ambo, wawe waangalifu wasije wakadaiwa kutumbukia kwenye msaibu.